MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemuhukumu  aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), David Mattaka na wenzake wawili kulipa jumla ya faini ya sh. Milioni kumi na mbili ama kutumikia kifungo cha miaka sita gerezani baada ya kupatikana na hatia katika makosa matano kati ya sita yaliyokuwa yakiwakabili likiwemo la kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 71.

Aidha mahakama imemuachia huru Mataka katika shtaka la moja la kuisababishia serikali hasara ya USD 42,459,316.12 kwa sababu kilelezo ambacho kilikuwa kinaonyesha kiasi cha fedha kilicholipwa kilichowasilishwa na shahidi wa upande wa Jamuhuri mahakamani hapo na kiasi cha fedha kilichopo kwenye hati ya mashtaka ni tofauti.

Hukumu hiyo  imesomwa leo Agosti 20,2021 na Hakimu Mkazi Mkuu Janet Mtega baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi 18 wa upande wa mashtaka.

Mbali na Mataka washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Dk Ramadhan Mlinga na aliyekuwa mwanasheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka. 

Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mtega amesema, upande wa mashtaka kupitia mashaidi wao wameweza kuthibitisha mashtaka yote dhidi ya washtakiwa pasipo kuacha shaka kuwa washtakiwa wametenda makosa yao. 

"Nimepitia ushahidi wote wa upande wa mashtaka na ule wa utetezi na ninawatia watuhumiwa wote hatiani katika mashtaka yote kasoro shtaka la tatu. 

Akisoma adhabu amesema, katika shtaka la kwanza mshtakiwa Mataka ambaye anakabiliwa na mashtaka manne peke yake anahukumiwa kulipa faini ya sh. Milioni nane na iwapo atashindwa atatumikia kifungo cha miaka minne gerezani huku washtakiwa Mlinga na Bertha wanatuhumiwa na shtaka moja tu la kughushi  watatakiwa kulipa faini ya sh. Milioni mbili kila mmoja  ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja kila mmoja gerezani iwapo watashindwa kulipa faini hiyo.

Kabla ya kusomwa adhabu kwa washtakiwa mahakama iliuuliza upande wa Jamhuri iliokuwa ukiongozwa na Wakili wa serikali  kutoka Takukuru Joseph Kiula kama walikuwa na lolote la kusema, ndipo Kiula akaifahamisha mahakama kuwa, mshtakiwa Mataka alishawahi kutiwa hatiani na kuhukimiwa katika kesi ya uhujumu uchumi  namba 277 ya mwaka 2011 na Hakimu Victoria Nongwa katika mahakama ya kisutu kwa mashtaka ya kula njama, matumizi mabaya ya madaraka na kusababisha hasara. 

Hata hivyo, wakili Kilua ameeleza kuwa hana kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa washtakiwa Mlinga na Berth. 

Akijitetea baada ya kutiwa hatiani ili asipewe adhabu kali, mshtakiwa Mattaka  ameiomba mahakama impunguzie adhabu kwani yeye ni mtu mzima sana wa miaka 70, pia anasumbuliwa na Tezi dume, shinikizo la juu la damu  na sasa anapata magonjwa mengine. Amedai kuwa kwa sasa anaishi na mke wake ambaye naye ni mgonjwa. 

Mshtakiwa Mlinga na Bertha kupitia wakili wao, Mpaya Kamala aliiomba mahakama kuwapunguzia wateja wake adhabu kwa kuwa ni wakosaji wa mara ya kwanza, mlinga anafamilia ya mke na watoto wanne ambapo kati yao wawili wanamtegemea. 

Kwa upande wa Bertha (57)Kamala alidai mteja wake huyo anasumbuliwa na shinikizo la juu la damu pamoja na mume wake ambao wanategemeana kwenye kuuguzana na pia ana wazazi ambao ni wazee na wanamtegemea yeye.

Katika hati ya mashtaka ilidaiwa, Oktoba 9, 2007 wakati Mattaka akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, alitumia madaraka vibaya kwa kusaini mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus na kwamba mkataba huo unadaiwa kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh. Bilioni 71.

Katika shitaka lingine Dk Mlinga na Soka walidaiwa kuwa Machi 19, 2008 katika ofisi za PPRA Ilala, Dar es Salaam walighushi muhtasari wa kikao wa tarehe hiyo, wakionesha kwamba mamlaka hiyo ilikaa kikao na kujadili maombi ya kuidhinisha ATCL ikodishe ndege hiyo.

Hata hivyo washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa faini na wameachiwa huru.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...