Na John Walter-Hanang

Katika kuhakikisha Vijana wenye vipaji katika michezo mbalimbali wanapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao,Mbunge wa Jimbo la Hanang mkoani Manyara Mhandisi Samwel Hayyuma ameanzisha ligi jimboni kwake aliyoipa jina la Mlima Hanang.

Mheshimiwa Hayuma amesema kuanzishwa kwa ligi ya michezo mbalimbali wilayani hapo kutasaidia kuinua vipaji ambavyo vinaweza kuwakilisha nchi katika mashindano mkubwa kama Olympic na pia kuhamasisha wanachi kutembelea hifadhi ya mlima Hanang mlima ambao unashika nafasi ya nne kwa urefu hapa nchini Tanzania ukiwa na mita 3103 ukiwa ni tofauti ya mita 1,463 na Mlima Meru unaopatikana mkoani Arusha. 

Akizungumza na waandishi wa Habari baada ya uzinduzi uliofanyika kata ya Endasaki, Mbunge huyo ameongeza kuwa ligi hiyo inahusisha michezo ya riadha mpira wa pete pamoja na mpira wa miguu hivyo amewahimiza wananchi kutoka maeneo mbali wajitokeze kwa wingi kushiriki katika michezo hiyo kwani michezo ni afya.

Timu kutoka kata 33 zimejitokeza kushiriki ligi hiyo ya mbunge (Mount Hanang Cup) huku mamia ya watu wakijitokeza kushangilia.Aidha katika kufanikisha mashindano hayo ametoa jezi pamoja na mipira ambapo wanufaika ni wachezaji kutoka kata zote 33 za jimbo la Hanang.
Amesema mashindano hayo yatakayokuwa yanafanyika kila mwaka, timu itakayoibuka mshindi itajinyakulia kitita cha shilingi laki mbili.

Akizungumzia mashindano hayo kiongozi wa Chama cha Soka wilayani humo na mwenyekiti wa mashindano hayo Mwalimu Charles William amesema hatua ya mbunge ya kuwakumbuka vijana ni ya kuungwa mkono na wadau wote wa michezo katika mkoa wa Manyara.
Amesema mashindano hayo yalianza katika ngazi ya vijiji na sasa ipo katika ngazi ya kata na baadaye katika ngazi ya Tarafa.

Aidha kwa upande wa washiriki wa mashindano hayo wamemshukuru Mbunge na kueleza kuwa ni fursa kwao kuonyesha vipaji walivyonavyo lakini pia inaimarisha ushirikiano baina ya vijana sanjari na kufanya afya zao kuwa bora zaidi.

Julius William ni mmoja wa washiriki hao amesema kuwa vijana wengi walikuwa wakikaa vijiweni mida ya jioni kwa kuwa hawakuwa na pa kwenda lakini kwa michuano hiyo watautumia muda wao kujishughulisha na michezo na kuacha kuwaza vitendo viovu.Michezo ni miongoni mwa ahadi aliyoitoa kwa vijana wa Jimbo la Hanang Mheshimiwa Hayyuma wakati akiomba kura mwaka 2020.

John Masatu mtumishi kutoka hifadhi ya Mlima Hanang amesema kupitia Michezo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwajulisha watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania na hata nje juu ya mlima huo wa kuvutia, kufika kutalii na kuiongezea nchi mapato.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...