Na Karama Kenyunko,Michuzi TV .


SERIKALI imetenga sh.bilioni 149 kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo Muswada unatarajiwa kupelekwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Septemba mwaka huu ili kuwa sheria rasmi.

Akizungumza leo mjini Dodoma wakati wa mkutano wa sita kati ya Wahariri na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao mwaka huu unasherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema wakati Watanzania wakijiandaa kuingia kwenye utaratibu wa bima ya afya kwa wote, Serikali imeona ni vema ikaanza kwa kutenga fedha hizo kufanikisha azma hiyo.

“Itaanza na wananchi wasio na uwezo kwa kugharamia matibabu na baadae itaendelea kupanua hadi itakapoweza kuwafikia watanzania wote. Ni matarajio yangu kuwa wahariri tutaibeba dhamira hii ya Serikali na kuhakikisha waandishi wetu wa habari wanaandika habari za kuhakikisha ajenda hii inafanikiwa ili watanzania waendelee kunufaika na huduma za bima ya afya,”amesema Msigwa.

Aidha ameipongeza NHIF kwa kupanua huduma za mfuko huo ambapo sasa pamoja na wafanyakazi , hata mtu moja mmoja ana uwezo wa kujiunga na mfuko. Pia amepongeza NHIF kwa kuviwezesha vituo mbalimbali vya kutolea tiba kuboresha huduma kwa kuvipatia mikopo ambayo inalipilika kwa urahisi.

Amesisitiza hilo ni jambo muhimu kwasababu mwisho wa siku nchi inakuwa na huduma bora za matibabu na kwa pamoja tutaweza kuokoa maisha ya wananchi walio wengi.Aidha amewaomba wahariri kuendelea kushirikiana na mfuko kutoa mchango wowote ambao wataona unafaa ili kuimarisha mfuko huo.

“Tunapokutana na taarifa zinazohusu huduma za afya tuwakumbuke watanzania wenzetu ambao wanataabika kupata huduma za matibabu kutokana na kukosa uwezo wa kulipia gharama za matibabu.Tutumie kalamu zetu kuhakikisha huduma za mfuko huu zinaimarika na zinaswanufaisha watanzania wengi zaidi”amesema Msigwa.

Akifafanua zaidi kuhusu mfuko huo  amesema yeye ni mwandishi wa habari hivyo anafahamu wahariri na waandishi wa habari wakiamua nchi hii iimbe wimbo wa bima ya afya wanaweza , wakiamua viongozi watoe umuhimu wa pekee kwa mfuko wa bima ya afya wanaweza.Wakiamua wadau wajitokeze waunge mkono mfuko huo wanaweza.“Wahariri ni muhimili imara ndani ya nchi na Serikali inawahaheshimu.”

Aidha amesema Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na mfuko huo tangu kuanza kwake mwaka 2001 katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa kila mtanzania licha ya kupitia changamoto lukuki lakini mfuko umeendelea kuimarika siku hadi siku.

“Kwa dhati ya moyo wangu naomba mniruhusu nikupongeze Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Benard Konga ,watumishi wa NHIF na Serikali kwa ujumla kwa kusimama kidete kuhakikisha mfuko huu unasonga mbele hadi leo hii unatimiza miaka 20 tangu uanzishwe.Tuliopita katika mapambano haya leo tunafarajika sana kuona mfuko huu sasa umekuwa kimbilio , kila mtanzania anataka kujiunga kwasababu sasa faida za mfuko zinaonekana dhahiri,”amesema Msigwa.

Amefafanua kwa wale ambao wamesahau ama hawakuwepo wakati mfuko huo unaanzishwa miaka 20 iliyopita amewaambia kuwa haikuwa rahisi .”Upinzani ulikuwa mkubwa sana , shukrani kwa msimamo thabiti uliowekwa na serikali kuwa ni lazima uanze , nakumbuka vyama vya wafanyakazi vilivyokuwa vikipinga watumishi kukatwa fedha kwa ajili ya kuchangia mfuko.

“Kuna wakati hata sisi waandishi wa habari tuliokuwa tunaandika kuhamasisha mfuko huu tulikuwa tunakata tamaa lakini tunashukuru leo tuko hapa tukifurahia mafanikio ya mfuko,”amesema Msigwa.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Benard Konga amesema mfuko huo ulipoanzishwa mwaka 2001 changamoto kubwa ilikuwa ni kukubalika hasa kwa sababu unahusisha kuchangia fedha lakini pia namna ulivyoanzishwa ,hivyo ilihitajika nguvu kubwa ya kuelimisha umma kuhusu dhana ya bima ya afya na umuhimu wake. Historia inaonesha mchango mkubwa uliofanywa na Wanahabari na Wahariri katika kuelimisha umma na hasa kwa sababu Mfuko uliwashirikisha sana.

Hivyo amesema lengo la kukutana na wahariri kwenye mkutano huo ni kutaka kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa kwa taasisi hiyo kwa miaka 20 ya uhai wa NHIF na kwamba itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha mfuko unaendelea kusonga mbele kwa mafanikio makubwa ya kutoa huduma za afya kwa watanzania wote.

Amesema mfuko huo kwa kipindi chote cha uwepo wake umekuwa na mchango mkubwa katika sekra ya afya kwani umefanikiwa kujenga majengo ya kutolea huduma za fya, umejenga hospitali na kununua vifaa tiba na kwamba mafanikio yote ambayo yanaonekana kwenye hospitali zote kubwa zikiwemo zile za rufaa nyuma yake kuna mkono wa NHIF katika mafanikio hayo.

Akifafanua zaidi sababu ya kikao hicho, Konga amesema lengo moja la kukutana siku ya leo ni katika kuadhimisha miaka 20 ya Mfuko tangu kuanzishwa kwa Mfuko pamoja na wahariri, aidha kama ilivyo ada  katika mkutano huo pia watapeana mrejesho ya yaliyofanyika katika kipindi chote hicho na kupata mrejesho kutoka kwa wahariri wa nini umma unapata kutoka kwao na kipi ambacho bado hakijakidhi mahitaji ya Watanzania.

Aidha Konga amesema mfuko huo umetoka mbali kiutekelezaji wa majukumu yake na  umeendelea kushirikiana na wadau wake katika kutekeleza hayo.”Kwa kuwa yataongelewa zaidi kwenye mada mimi nagusia kidogo tu. Tunapoongelea tulipotoka na tulipo tunaweza kuongelea haya: Wote sasa wamewekewa utaratibu wa kujiunga na Mfuko tofauti na hapo awali ambapo makundi machache na hasa watumishi ndio waliwezeshwa kujiunga.

“Tumewezesha vituo mbalimbali kuimarisha huduma za matibabu na miundombinu kupitia mikopo nafuu inayotulewa na NHIF. Vituo kama MNH, MOI, KCMS, BMH na vingine ni wanufaika,Malipo kwa Watoa huduma yamewezesha vituo kuwa na mapato ya uhakika ambayo yanawezesha vituo kuimarisha huduma,”amesema Konga.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akikata keki huku akishudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Biama ya Afya (NHIF), Bernard Konga (katikati) na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ikiwa ni ishara ya kudumisha ushirikiano wakati wa mkutano wa sita kati ya Wahariri na NHIF ambao mwaka huu unasherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Mkutano huo umefanyika leo Agosti 28, 2021 jijini Dodoma.


Msemaji Mkuu wa Seikali ambaye ni Mgeni rasmi katika mkutano huo, Msigwa (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Konga (kushoto) na Mwenyekiti wa TEF, Balile wakibadilishana keki kabla zingine kuzigawa kwa wahariri na waandishi wa habari waliokuwepo wakati mfuko huo unaanzishwa mwaka 2001.


Baadhi ya wahariri waliokuwepo wakati NHIF inaanzishwa mwaka 2001 wakikagawiwa keki


Baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari nchini wakionesha keki hizo baada ya kugawiwa. Baadaye wahariri wote waliohudhuria mkutano huo walikula keki hiyo.
Meneja Uhusiano wa NHIF, Anjela Mziray akizungumza neno la utangulizi wakati wa kuanza mkutano huo.


Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga akielezea historia ya mfuko huo ulioanzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu mwaka 2001.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
 

Sehemu ya wahariri wa vyombo vya habari wakiwa makini kusikiliza yaliyokuwa yanajiri mkutanoni.

 

Baadhi ya maafisa wa NHIF wakiwa katika mkutano huo ambapo baadhi walijibu maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wahariri kuhusu mfuko huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...