WAZAZI nchini wamehimizwa kuweka mkazo katika kuwapatia watoto wao lishe bora ikiwemo kuhakikisha wanakunywa maziwa kila wakati ili kuwafanya wawe na afya nzuri itakayowasaidia kufanya vizuri katika masomo yao.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Asimwe Rwiguza wakati akizindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Unywaji Maziwa Shuleni uliyofanyika Mkoani Kilimanjaro Agosti 27, 2021.

Wakati akizindua kampeni hiyo Dkt. Rwiguza amesema kuwa jukumu la lishe lipo mikononi mwa wazazi hivyo ni muhimu wakajitahidi kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kugharamia lishe ya watoto  wao.

"Natoa wito kwa wazazi wote nchini kuona umuhimu wa kuwapa maziwa watoto,  faida za unywaji wa maziwa kwa watoto zinafahamika sitaki kuzirudia hapa, maziwa yatawajenga, watakuwa na akili na kuwasaidia kufanya vizuri katika masomo yao," Amesema Dk Rwiguza

Aliongeza kuwa uzinduzi huo wa awamu ya pili uwe chachu kwa jamii kuhakikisha watoto wao wanakunywa maziwa ya kutosha na zile changamoto zilizoonekana wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika awamu ya kwanza zishughulikiwe ili mafanikio yaweze kupatikana.

Naye,  Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk George Msalya amesema kuwa kufuatia uzinduzi wa kampeni hiyo ni muhimu sasa kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika uchakataji wa maziwa ili kufanya maziwa hayo kupatikana kwa wingi na wakati wote hatua ambayo itawawezesha wawekezaji  kukuza uchumi wao na wa nchi kwa ujumla.

"Maziwa yanayoingia katika mfumo rasmi wa uchakataji katika Viwanda vyetu ni chini ya asilimia 3 ya maziwa yote yanayozalishwa hapa nchini, hiyo ni asilimia ndogo ukilinganisha na nchi za wenzetu, hivyo ni muhimu kuhamasisha wawekezaji ili kukuza tasnia hii ya maziwa nchini," Amesema Dk Msalya

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Ushirika cha Wanawake, Nronga, kinachojishughulisha na uchakataji wa Maziwa Mkoani Kilimanjaro, Hellen Ussiri amesema kuwa baada ya Serikali kutoa tamko la uhamasishaji wa unywaji wa maziwa shule bado kumekuwa na mwamko mdogo hivyo Chama hicho kimefanya jitihada za kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha unywaji wa maziwa shuleni.

"Kiwanda cha Nronga kitasambaza maziwa kwa shule 10  za msingi zilizopo katika Wilaya ya Hai zenye jumla ya Wanafunzi 6151 ili kuendelea kutoa hamasa ya Unywaji wa maziwa kwa watoto," Amesema Ussiri.

Aidha, alitoa rai kwa wadau mbalimbali wa biashara  pamoja na wazazi kwa ujumla kuunga mkono juhudi hizo ili walau adhma ya kuwapatia watoto wa shule maziwa mara mbili kwa wiki iweze kufanikiwa.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dk Asimwe Rwiguza (kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Juma Said Irando (katikati) pamoja na Katibu wa Chama cha Ushirika cha Wanawake, Nronga, Hellen Ussiri kwa pamoja wakinywa maziwa ikiwa ni ishara ya kuzindua Awamu ya Pili ya Unywaji wa Maziwa Shuleni katika Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro Agosti 27, 2021. Katika Uzinduzi huo Dkt. Rwiguza aliwahimiza wazazi kuzingatia lishe bora kwa watoto wao ikiwa ni pamoja na kuwapa maziwa kila mara ili kujenga afya zao.
Mmoja wa Maafisa wa Chama cha Ushirika cha Wanawake Nronga akigawa maziwa kwa Wanafunzi waliohudhuria tukio la Uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Unywaji wa Maziwa Shuleni liliyofanyika Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dk Asimwe Rwiguza akiongea na Wadau waliohudhuria uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Unywaji wa Maziwa Shuleni iliyofanyika Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro.
Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk George Msalya akitoa maelezo mafupi kuhusu maendeleo ya tasnia ya Maziwa nchini wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Unywaji wa Maziwa Shuleni iliyofanyika Wilayani Hai, Mkoani Kilimanjaro.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...