Na Mwaandishi Wetu Mtwara

TAASISI ya Benjamini Mkapa kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Mtwara chini ya ufadhili wa Shirika la UNICEF imetoa mafunzo kwa wahudumu wa ngazi ya jamii 194 kutoka Newala na Nanyamba Mji ili waweze kuwa kiungo katika utoaji wa huduma za afya kati ya jamii na vituo vya afya vilivyopo maeneo yao.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku 16 kwa wahudumu hao, Ofisa Miradi kutoka Taasis ya Benjamin Mkapa Zawadi Dakika amesema wahudumu hao wamepewa mafunzo ambayo yatawawezesha kutoa elimu ya afya katika jamii yao ili kusaidia kuimarisha afya ya jamii hususani katika afya ya lishe na uzazi.

“Tumechagua  Newala na Nanyamba kwa sababu ilionekana kwamba kuna tatizo kubwa la udumavu na ‘malnutrition’ kwa watoto katika halmashauri zote mbili, kwa hiyo tumewaweka wahudumu hawa ili waweze kusaidia kuelimisha jamii namna bora wanaweza wakatumia vyakula vilivyopo kwenye jamii kuimarisha afya zao,” amesema.

Ameongeza kwa siku 16 wahudumu hao wamefundishwa jinsi ya utoaji wa elimu ya afya katika ngazi ya jamii, jinsi ya kutoa elimu ya afya ya lishe na kutoa rufaa kwa wagonjwa pale wanapoona wanahitaji kwenda kituo cha afya.

Amesema mafunzo hayo yanafanyika katika mikoa takribani kumi nchini ambapo Taasis ya Benjami Mkapa inatekeleza miradi ya kuimarisha afya ya lishe katika jamii.

Kwa upande wakeaimu Mnganga Mkuu wa Halmashauri ya Newala Mji Kidei Mzerela ameishukuru Taasis hiyo ya Mkapa kwa kuchagua Mji wa Newala ambayo amesema yatasaidia kuibua wahitaji wa hudumu za lishe kama vile watoto, wajawazito na wazee.

“Tumekuwa tunapata changamoto ya kuwafikia wahitaji wa huduma za afya kwenye upande wa lishe kama vile watoto na wajawazito, watoto wengi wanakuja kupata huduma za afya wakiwa tayari wana viriba tumbo, tatizo limeshakuwa sugu na inakuwa ngumu kuwatibu,” amesema.

Mzerela amesema kupitia mradi huu wa Mkapa wahudumu waliopewa mafunzo wataweza kuwaibua watoto wenye tatizo la lishe na wajawazito ambao hawaji kiliniki kwa wakati.

Amesema pia kupitia hiyo program ya Taasis ya Mkapa, wahudumu waliopewa mafunzo katika Mji wa Newala wataweza kuwaibua wagonjwa wenye tatizo la TB ambao pia imekuwa ngumu kuwafikia katika jamii.

Aidha Ofisa Lishe wa Mkoa wa Mtwara Harriet Kipuyo amesema Mkoa umekuwa ukifanya jitihada za kupunguza tatizo la lishe ambapo kwa sasa wameweza kupunguza udumavu kwa watoto kutoka asilimia 44 na kufikia asilimia 30 kwa mwaka 2020/2021.

Amesema kwa Newala na Nanyamba bado kuna changamoto kubwa ambapo kwa Newala tatizo la udumavu kwa watoto lipo kwa asilimia 10 na Nanyamba asilimia 11.

Amesema mafunzo wahudumu waliochaguliwa na kupewa mafunzo watasaidia jamii kujikita zaidi katika kuhakikisha lishe bora kwa watoto na jamii nyinging ili kufikia lengo la mkoa huo kupunguza tatizo mpaka kufikia asilimia 5 kwa Newala na Nanyamba TC.

Amesema sababu kubwa inayochangia udumavu kwa Mkoa wa Mtwara ni mila na desturi ambapo watu wazima wanakula pamoja na watoto bila kufahamu kuwa watoto wanahitaji chakula chao maalum chenye lishe bora.

“Kuna tatizo la mila na desturi linachangia sana, mtoto hapewi kipaumbele, wanakula na watu wazima bila kujua mtoto anatakiwa kula nini,” amesma.



Wahudumu ngazi ya jamii Wilaya ya Newala wakiwa wanajifunza jinsi ya kuandaa chakula cha Lishe Bora Kwa watoto na wajawazito ikiwa ni sehemu ya mafunzo waliopewa na Taasisi ya Benjamin Mkapa Kwa kushirikiana na mamlaka ya Mkoa wa Mtwara


Vifaa vya kazi mbalimbali ambavyo vilitolewa na Taasisi ya Benjamin Kwa ajili ya kuwawezesha wahudumu hao wa afya ngazi ya jamii kutekeleza majukumu Yao katika utoaji wa Elimu ya Lishe na Afaya ya Uzazi kwenye maeneo yao
Wahuduma wa afya ngazi ya jamii kutoka Halmashauri ya Newala wakiwa kwenye mafunzo ambayo yalilenga kuwawezesha kutoa Elimu kwenye maeneo Yao ilo kusaidia jamii kuimarisha afya ya Lishe na Afya ya uzazi. Mafunzo hayo yalitolewa na Taasisi ya Benjamin Mkapa Kwa kushirikiana na mamlaka ya Mkoa wa Mtwara chini ya Ufadhili wa Shirika la UNICEF.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...