Charles James, Michuzi TV

SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Canada zinatarajia kukamilisha mradi wa kuboresha Vyuo vya Ualimu Nchini unaoitwa 'Upgrading Teachers Colleges UTC' katika Vyuo vinne vya Mpuguso, Shinyanga, Kitangula na Ndala ifikapo Juni 2022.

Mradi huo wa UTC ambao ulianza Mwaka 2016 unatekelezwa kwa ushirikiano wa Nchi hizi mbili ambapo umelenga kufanya maboresho katika miundombinu ya Vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kukarabati majengo yaliyokuepo na kujenga mengine mapya.

Akizungumzia mradi huo mbele ya wandishi wa habari waliofika katika Chuo Cha Mpuguso kilichopo Wilayani Rungwe Mkoani Mbeya, Mshauri Elekezi wa UTC, Mhandisi Renatus Dominick amesema kiasi kinachotumika kwenye kukamilisha mradi huo kwenye vyuo hivyo vinne ni Sh Bilioni 39 ambazo Serikali ya Tanzania inatoa Sh Bilioni 8.2 huku Canada wenyewe wakitoa Sh Bilioni 30.

" Huu mradi unaitwa The Upgrading Teachers Colleges UTC ulianza mwaka 2016 kwenye vyuo hivi vinne vya Ualimu Nchini na tunarajia kukamilisha Juni 2022, lengo la mradi huu ni kuboresha mazingira ya vyuo hivi ambavyo vingi ni vyuo vya zamani ambavyo tayari majengo yake yalishachakaa, mpaka sasa tumeshapokea kiasi cha Sh Bilioni 29 kutoka Serikali ya Canada kwa ajili ya mradi huu," Amesema Mhandisi Renatus.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hiko cha Mpuguso, Nathaniel Hinju ameishukuru Serikali kwa kuwezesha kufanyika kwa maboresho hayo ambayo ameeleza kuwa yatakua na faida kubwa ikiwemo kuboreka kwa mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kutokana na uwepo wa maabara, maktaba na madarasa mengine mapya.

"Zipo faida nyingi za maboresho ya mradi huu, ulinzi na usalama umeimarika kutokana na kupata umeme wa Sola, ongezeko la matanki ya kuhifadhia maji, uwepo wa ukumbi umetoa fursa kubwa ya kufanya mabaraza ya chuo kwa ufanisi zaidi pamoja na wanafunzi kunufaika kusoma masomo ya Sayansi kwa vitendo," Amesema Hinju.

Amesema sababu zilizopelekea kuomba mradi huo ni uchakavu na upungufu wa miundombinu kutotosheleza kufuatana na mahitaji, ongezeko la udahili wa wanachuo uliotokana na matokeo mazuri ya mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari MMES na maoni ya chuo kuendesha kozi za Sayansi

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo amesema ujenzi na ukarabati wa Chuo hicho ulianza mwaka 2016 na ulihusika katika ujenzi wa nyumba nne za watumishi, tatu zikiwa za ghorofa moja zenye uwezo wa kuishi watumishi 13, ujenzi wa mabweni mawili yenye ghorofa moja moja yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 304, ukumbi wa mikutano na ukarabati wa nyumba nne za watumishi.

Mradi huo pia umegusa ujenzi wa majengo mawili ya madarasa yenye ghorofa moja moja ambapo madarasa hayo yana uwezo wa kuchukua wanachuo 720, jengo la mhadhara, maabara, maktaba na ukarabati wa mabweni mawili na choo cha wasichana.

" Tunaishukuru sana Serikali yetu chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kuboresha mazingira yetu ya kufundishia na kujifunzia," Amesema Hinju.

Nae Rais wa Chuo hicho, Mussa Bilauri ameishukuru Serikali kwa maboresho hayo ambayo yataongeza chachu ya wao kuzidi kujisomea lakini pia kufungua mwanya kwa Chuo kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi na hivyo kuongeza uzalishaji wa idadi kubwa ya Walimu nchini.

Muonekano wa picha za nyumba za watumishi katika Chuo Cha Ualimu Mpuguso Wilayani Rungwe, Mbeya ambazo zimepitiwa na mradi wa UTC.

Muoenekano wa picha za majengo mawili ya madarasa katika Chuo Cha Ualimu Mpuguso Wilayani Rungwe Mbeya ambazo zitakua na uwezo wa kuchukua wanafunzi 720.
Hili ni bweni la wanafunzi wa kiume katika Chuo Cha Ualimu Mpuguso liliopewa jina la Magufuli ambalo utekelezaji wake umefanywa kupitia mradi wa UTC.
Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Mpuguso Wilayani Rungwe, Nathaniel Hinju akizungumza na wandishi wa habari kuhusiana na maboresho makubwa ya miundombinu yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia chuoni hapo.

 Mshauri Elekezi wa UTC Mhandisi Renatus Dominick akizungumza na wandishi wa habari kuelezea hatua ambazo miradi hiyo imefikia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...