Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Mhe. Othman Masoud Othman,
amewahimiza wanachama wa chama hicho kuendelea kuunga mkono juhudi za
viongozi wao ili waweze kufikia dhamira yao.
Ameyasema
hayo katika kikao maalumu pamoja na viongozi wa ACT Wazalendo wa mikoa
yote saba ya kichama ya kisiwani Unguja kilichofanyika kwenye Ukumbi Wa
Majid Hall, uliopo Kiembe Samaki, Magharibi 'B' Unguja.
“Kwa
kweli, nafasi pekee ya kukifikisha chama chetu katika dhamira yake ni
kwa wanachama kuendelea kuunga nguvu moja katika utafutaji wa haki
pamoja na kuwa na umoja wa dhati na mshikamano”, alisema Mhe. Othman,
ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Aidha,
amesema ni muhimu kuendelea kujenga hoja madhubuti, nidhamu pamoja na
uwajibikaji kama misingi ya kukiendeleza chama hicho.
Amesisitiza
kuwa misingi bora iliyoachwa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho,
Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, imekuwa ni fursa kwa chama kuendelea
kuungwa mkono na wananchi walio wengi nchini, jambo linalotoa taswira
mpya katika kufikia dhamira yao.
“Heshima
aliyotuwachia Mzee wetu ndiyo ambayo hadi leo inatubeba na kutuweka
mbele ya wengine na hivyo lazima kwetu kuendelea kuienzi,” alisema.
Sambamba
na hayo, amewakumbusha wanachama hao kuendelea kudumisha amani ya kweli
na uwajibikaji kwa lengo la kuinua maendeleo ya Zanzibar.
Mapema
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Ndugu Zitto Zubeir Kabwe, amesema Chama
hicho kitaendelea kuhakikisha makubaliano yaliyopo baina yao na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yanatekelezwa ikiwemo suala la
uchunguzi juu ya waathirika wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, uwepo wa
tume ya maridhiano itakayotoa haki sawa kwa raia wote pamoja na kuwepo
kwa chaguzi za haki nchini.
Ameongeza
kuwa kuwepo kwa Katiba Mpya ni miongoni mwa fursa pekee itakayoiinua
Zanzibar kimaendeleo pamoja na kuondosha matatizo mbalimbali
yanayojitokezaa katika kila chaguzi zitakazofanyika nchini.
Kikao
hicho kimekamilisha ziara ya viongozi wa chama hicho iliyoanza tarehe 9
Agosti huko kisiwani Pemba, ambapo kwa ujumla wamekutana na viongozi wa
Mikoa 11 ya kichama, Majimbo 50 pamoja na Matawi 682 ya chama hicho
kwa Unguja na Pemba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...