Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Zikiwa zimebaki siku chache kufungwa dirisha la usajili na uhamisho wa Kimataifa kwa Klabu za Tanzania, Miamba ya Soka nchini, Yanga SC, Simba SC na Azam FC imeendelea kutikisa  na kugonga Vichwa vya Habari vya Michezo kwenye usajili huo kwa ajili ya msimu ujao wa Mashindano wa 2021-2022.

USAJILI WA YANGA SC; WAKONGO KUWABEBA WANANCHI MSIMU UJAO

Yanga SC wamenaka kupania msimu ujao wakiendelea kufanya usajili kabambe ili kuimarisha Kikosi chao kwa Wachezaji mbalimbali wa Kimataifa. Yanga wameshusha Wakongo wengi katika Kikosi chao kina, Fiston Mayele, Shaaban Djuma na Heritier Makambo wakiungana na wenzao kina Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda.

Wakiwa tayari wamekosa Ubingwa wa Tanzania Bara misimu minne mfululizo, Yanga SC wametajwa kufanya usajili wa Konde Boy kutoka Msumbiji katika Klabu ya UD Songo, Jimmy Ukonde (Julio) aliyetajwa kutua kwa Wananchi kwa ajili ya msimu ujao. Pia Yanga SC wamefanya usajili wa Wachezaji wa Ligi ya nyumbani Tanzania, wamesajiliwa kina Dickson Ambundo, Yusuph Athumani.

Usajili huo wa Yanga SC ni wazi wanania ya kufanya vizuri na kuleta ushindani katika Mashindano mbalimbali ikiwa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) ambayo wanashiriki msimu huu unaoanza September mwaka huu.


USAJILI WA SIMBA SC NA KUFURU YA UHAMISHO WA MIQUISSONE


Wekundu wa Msimbazi, Simba SC kwao wamekamilisha usajili wa Mchezaji wa Kimataifa wa Malawi na Klabu ya Nyasa Big Bullets FC, Peter Banda kwa mkataba wa miaka mitatu akitajwa kuwa mrithi wa Mchezaji Luis Jose Miquissone ambaye ametajwa kutimkia Al Ahly SC ya Misri.


Hata hivyo, Simba SC imeeleza kufanya usajili wa Kisayansi kujipanga mathubuti kwa ajili ya msimu ujao wa Mashindano. Idadi ya Wachezaji wa Simba SC wengi wamekaa pamoja muda mrefu na kuzoeana Kikosini, licha ya kumsajili Banda wa Malawi, Simba SC pia wamehusishwa na usajili wa Kiungo Mkabaji wa Kimataifa wa Uganda (The Cranes), Khalid Aucho kutoka Klabu ya Makkasa SC ya Misri, Kiungo ambaye ametajwa pia kusajiliwa na Yanga SC kwa tetesi.


Tetesi na fununu zinaeleza kuwa tayari Mnyama mkali amefanya usijali kwa idadi kubwa ya Wachezaji wa Ligi ya nyumbani ambao msimu uliopita walicheza timu mbalimbali katika Ligi Kuu. Tetesi zinasema katika usajili huo wapo, Mshambuliaji Dennis Kibu kutoka Mbeya City, Kiungo Abdul Swamad wa Kagera Sugar, Golikipa Jeremiah Kisubi wa Tanzania Prisons, Beki Israel Patrick Mwenda wa KMC na Jimmyson Mwanuke wa Gwambina.


Wakati huo, Simba SC Mchezaji wao machachari, Luis Jose Miquissone ametajwa kuondoka Klabuni hapo na kusajiliwa Al Ahly SC ya Misri kwa mkataba uliovunja rekodi ya usajili nchini wa Bilioni 2 za Kitanzania.


USAJILI WA AZAM FC KULETA KIKOSI CHA USHINDANI MSIMU UJAO

Azam FC wamefanya usajili wa kutosha kwa ajili ya msimu ujao, wamefanya usajili mkubwa wa Washambuliaji wengi tishio katika Soka la Afrika. Wamesajili Mshambuliaji nguli wa DR Congo, Idriss Mbombo kutoka Klabu ya El Gouna ya Misri, pia yupo Mzambia Paul Katema kutoka Klabu ya Red Arrows ya nchini humo, Kiungo Mshambuliaji wa Kimataifa wa Kenya, Kenneth Muguna kutoka Gor Mahia ya huko huko Kenya.


Wengine ni Mshambuliaji wa Kimataifa wa Zambia, Rodgers Kola kutoka Klabu ya Zanaco  ya nchini humo, pia imemsajili Beki wa pembeni wa Kimataifa wa Tanzania, Edward Charles Manyama kutoka Ruvu Shooting FC ya hapa nchini. Wauza ‘Ice Cream’ kutoka Chamazi wameenda Zanzibar kukamilisha uhamisho wa Golikipa wa KMKM, Ahmed Ali Suleiman ‘Salula’ kwa mkataba wa miaka miwili.

Wapo Wachezaji ambao Azam FC waliwatoa kwa mkopo katika Klabu mbalimbali, Wachezaji hao, Mshambuliaji Paul Peter, Kiungo Masoud Abdallah (Cabaye), Beki Lusajo Mwaikenda waliokuwa KMC FC, Idd Kipagwile aliyekuwa Namungo FC na Tepsie Evancy, Samwel Jackson Onditi waliokuwa Ihefu SC wakizitumikia timu hizo kwa mkopo.


Timu mbalimbali za Ligi Kuu Soka Tanzania Bara zimeendelea kufanya usajili ili kuimarisha vikosi vyao kuelekea msimu ujao wa Mashindano huku dirisha la usajili likitarajiwa kufungwa 31 Agosti, 2021.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...