Na Karama Kenyunko-Michuzi TV

Vigogo watano wa zamani wa Mamlaka ya Vitambulisho ( NIDA) wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mbali mbali kiwemo shtaka la kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 1.175 wamekutwa na kesi ya kujibu na wataanza kujitetea.

 Washtakiwa hao ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) Dickson Maimu, aliyekuwa Mkurugenzi wa Sheria wa mamlaka hiyo, Sabina Raymond, Meneja wa Biashara, Xavery Kayombo, Aveln Momburi na George Ntalima.

Uamuzi huo, umetolewa leo Agosti 12, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashi Chaungu, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 26 wa upande wa Jamhuri na vielelezo 45 na kujiridhisha kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu.


Akisoma uamuzi huo, Hakimu Chaungu amesema, kwa mara ya kwanza washtakiwa walisomewa mashtaka 55 yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, matumizi mabaya ya madaraka, kutakatisha fedha makosa 10 na kutumia nyaraka kumdanganya muajiri makosa 25.

"Nimepitia ushahidi wa mashahidi wote 26 na upande wa Jamhuri na vielelezo 45, nimeridhika kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu, kwa hiyo mtatakiwa kusema mtajitetea kwa njia gani, mna mashahidi wangapi na  vielelezo vingapi amesema na kuuliza Hakimu Chaungu.

Kufuatia hayo, Wakili anayemtetea Maimu, George Nduguru amedai mteja wake atajitetea kwa kiapo na pia wataleta mashahidi sio chini ya 20 na vielelezo sio chini ya 10 huku mshtakiwa wa pili Momburi,  Wakili wake Kung'e Wabeya amedai mteja wake atajitetea kwa kiapo na atakuwa na mashahidi watano pamoja na yeye mwenyewe na vielelezo.

Pia mshtakiwa watatu Kayombo, atajitetea kwa kiapo na kuleta mashahidi watano na vielelezo 10 huku mshtakiwa Ntalima, akileta mashahidi wanne, vielelezo saba na atajitetea kwa kiapo na kwa upande wa mshtakiwa Raymond amedai atakuwa na mashahidi wawili na vielelezo visivyozidi sita.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 25 na 26, 2021 itakapoitwa kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea.

Mapema shahidi wa mwisho katika kesi hiyo,Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),  Emmanuel Koroso, amedai kuwa Mkurugenzi wa Sheria wa Mamlaka hiyo, Sabina Raymond alishuhudia  utiwaji saini mkataba ulioiingizia serikali hasara ya Dola za Marekani 551,500.

Akiongonzwa na Wakili Ladislous Komanya, Koroso alidai wakati akifanya nahojiano na Sabina alimweleza kuwa yeye ndiye alikuwa msimamizi wa masuala yote yanayohusu sheria NIDA ikiwemo kusimamia na kushuhudia utiwaji saini wa mikataba mbalimbali.

Koroso alidai Mlmkataba wa Dola za Marekani 551,500 ulikuwa kati ya NIDA na Kampuni ya Ms Law Partner in Association of School of Law Tanzania of University of Dar es Salaam kwa ajili ya mapito ya sheria katika utekelezaji wa mradi huo na kulipwa kiasi hicho cha fedha na NIDA.

Alidai fedha hizo hazikupaswa kulipwa na NIDA  bali  Kampuni ya Gotham International Ltd ambayo iliingia mkataba wa Dola za Marekani 9,000,000  na NIDA kwa ajili ya kazi ya vitambulisho ikiwemo kutoa ushauri elekezi katika utekelezaji wa mradi wa NIDA.

Alidai pia mshtakiwa huyo alimueleza kwamba katika mkataba huo, Gotham ilikubaliana na NIDA kuwa inaweza kufanya kazi hiyo yenyewe ama kutafuta mtu  au Kampuni kwa malipo hayo.

Alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba huo NIDA haikupaswa kulipa Dola za Marekani  551,500 bali fedha hizo zilitakiwa zilipwe na Gotham, moja ya majukumu ya Sabina ilikuwa kusimamia utekelezaji wa mkataba huo katika maeneo ya sheria.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...