Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dkt. Amos Nungu akiwa katika picha ya pamoja na wabunifu kutoka kampuni changa mbali mbali wakati wa mkutano wao ili kupata wawakilishi wawili watakaoenda nchini Finland kushiriki mashindano ya kimataifa ya kutoa mawazo yao kuona kama yanaweza kufadhiliwa na kupata mafunzo zaidi.
Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Dkt. Amos Nungu akizungumza na wabunifu kutoka kampuni changa mbali mbali wakati wa mkutano wao ili kupata wawakilishi wawili watakaoenda nchini Finland kushiriki mashindano ya kimataifa ya kutoa mawazo yao kuona kama yanaweza kufadhiliwa na kupata mafunzo zaidi.

 

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amewataka vijana wabunifu waliyokuwa kwenye kampuni changa kutoridhika na kile walichonacho badala yake, waendelee kujifunza na kudadisi.

Dkt. Nungu amesema hayo leo Agosti 19,2021 jijini Dar es Salaam, wakati alipokuwa akizungumza na vijana kutoka katika kampuni changa, kwa lengo la kupata washindi wawili watakaokwenda kushiriki kwenye mashindano ya Kimataifa ya kutoa mawazo yao kuona kama yanaweza kufadhiliwa na kupata mafunzo zaidi.

Amesema katika mafunzo hayo, eneo moja ni la kusaidia vijana kwenda Finland na eneo lingine ni kushindanisha makampuni machanga kwa ajili ya  kutoa huduma zao ndani ya nchi washirika.

Amesema, vijana wengi waliokuwa katika kampuni hizo wanakuwa na mawazo ya kuchangia kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini ndiyo maana tume inawakusanya kwa pamoja ili kuendeleza mawazo yao.

Mkurugenzi huyo, alisema katika mchakato huo walipokea maombi 79 ambapo, walifanya mchujo na kubakia kampuni baadhi ambazo zitashindanishwa na kupatikana kwa washiriki wawili watakaoenda Finland.

"Tulifanikiwa kupata makampuni zaidi ya 10 ambayo yaliweza  kushindana na kushinda kwa kupata ufadhili kwa kushirikiana na wenzao katika hilo tunajivunia kampuni ya Arusha na Filter ambao wao walipata ufadhili wa kupeleka teknolojia yao nchini Zambia, kupitia mradi huu wa  SAIS,"

"Katika miradi hiyo zaidi ya 10, miwili ilikuwa inalenga kusaidia vijana wa kike na wa kina mama kushiriki katika masuala ya Tehama," alisema Dkt. Nungu.

Alisema mchakato huo upo chini ya Mradi wa Kukuza Ubunifu Kusini mwana Afrika (Southern African Innovation Support Program -SAIS, ambapo hapa nchini Costech ndiyo msimamizi wa mradi huo.

Dkt. Nungu alisema mradi huo unaofadhiliwa na Serikali ya Finland umeanza, 2017 na una wakilishwa nchi ya Tanzania, Botswana, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia pamoja na SADC , lengo ni kujenga mifumo ya ubunifu ndani ya nchi zilizokuwepo katika mradi huo na pia kujenga ushirikiano katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Kwa upande wake, muanzilishi na Mwanasayansi wa bahayu kutoka kampuni inayojihusisha na shughuli za uchakataji taka za plastiki kwenda kwenye vifaa vya ujenzi (Arena Recycling Industry,)Hallas David amesema mafunzo ya mradi huo yanayotolewa na Costech yamewawezesha kuweza kufika mbele kwa kuboresha zaidi bunifu zao ili baadae zije kusaidia katika ukuaji wa teknolojia na uchumi nchini.

"Tunafurahi kuona Serikali na SAIS ikiwasaidia vijana wenye mawazo na wabunifu ambao wanatatua changamoto zilizopo ndani ya mazingira yetu na jamii ili kuweza kujiinua kiuchumi na kulipatia Taifa uchumi endelevu,"

"Nashukuru sana kwa hatua tuliyofikia, tumeweza kupata mafunzo mbali mbali yatakayotuwezesha sisi kuendelea kufika mbali zaidi na mawazo yetu kwa kutukutanisha na watu mbali mbali wanaotupa ushirikiano na misaada katika kazi zetu za ubunifu pamoja na masoko na vifaa," alisema David.

Alisema, kama wakipata kibali cha kuiwakilisha nchi, nchini Finland itakuwa ni furaha zaidi kwako na wataonesha kuwa Tanzania kuna wabunifu wanaofanya vizuri katika sayansi na teknolojia.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...