Na. Mwandishi Wetu.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ubungo Mh. Jafari Juma   amepongeza wakala wa Mabasi yaendayo Haraka DART kwa kusimamia mradi wa ujenzi wa Kituo kidogo na karakana ya Mabasi Yaendayo Haraka kilichojengwa ilipokua stendi kuu ya Mabasi ya mikoani eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam.

Katika ziara yake na Madiwani wa Manispaa ya Ubungo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi hususan katika eneo la miundombinu, Meya Jafari  alisema amefurahishwa na jinsi Wakala ulivyosimamia ujenzi wa kituo hicho ambapo amesema thamani halisi ya fedha inaonekana na kituo kimebadilisha taswira ya eneo hilo na kuwa pakuvutia.  

“Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi thabiti wa Mh. Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan imeendeleza ujenzi pamoja na kukamilisha miradi ambayo iliasisiwa na awamu zilizopita lengo ikiwa ni kuwapunguzia kero wananchi” Alisema.

Amesema mradi wowote ambao haujasimamiawa vizuri kabla haujakabidhiwa, huanza kuonyesha mapungufu ikiwemo kukatika, kupinda kwa baadhi ya kuta na wakati mwingine hata mabati kuvuja ila kwa mradi wa kituo kidogo na karakana ya Ubungo Wakala umetenda haki na umeitoa kimasomaso Serikali.

“Kwenye ukweli lazima tuseme, ambaye alikua hapajui hapa kabla ya ujenzi akifika hapa atashangaa sana, huu ni mradi mzuri sana ambao sisi wakazi wa Manispaa ya  Ubungo tunajivunia” Alisema.

Kwa upande wake mhandisi Mohamed Kuganda kutoka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka DART, alisema kituo hicho kidogo  na karakana vimekamilika kwa asilimia 99 na kinachosubiriwa ni mkandarasi kurekebisha baadhi ya mapungufu madogo katika miundombinu ili aweze kukabidhi.

“Tumefanya ukaguzi wa jinsi Mabasi yatakavyoweza kuingia na kutoka hapa kituoni, pia tumekagua na kujaribisha mabasi kuingia kwenye mashimo maalumu ya kufanyia matengenezo na tumeshauri yafanyiwe marekebisho kidogo ili mabasi yaweze kuingia kwa urahisi” Alisema Mhandisi kuganda.

Kituo kidogo na karakana ya  Ubungo kina uwezo wa kuegesha Mabasi zaidi ya 80 na lengo la Wakala kukijenga ni kupunguza uhaba wa sehemu ya kulaza na kuegesha mabasi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya Mabasi na pia kupunguza msongamano eneo la Karakana na kituo cha  Jangwani.

Aidha kituo hicho kitakuwa kituo unganishi kati ya abiria wanaotoka katika njia ya awamu ya kwanza ambayo ni kuanzia Kimara hadi Kivukoni na Gerezani, ikiunganisha na awamu nyingine zitakazopita katika barabara za Mandela, Sam Nujoma hadi Tegeta.

Mstahiki Meya Mheshimiwa Jafary Juma na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wakipokea maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kidogo na Karakana ya Mabasi Yaendayo Haraka Ubungo ilipokuwa Stendi Kuu ya Mabasi ya Mkoani, tarehe 9/9/2021.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...