NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za Vitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya kuhakikisha wanaunda kamati za maridhiano kwa ajili ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza katika baadhi ya maeneo na kuleta madhara kwa jamii.

Ulega alitoa agizo hilo kwenye ziara aliyoifanya katika Kijiji cha Nakiu Kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi Septemba 13, 2021 baada ya kupokea kero zilizohusu migogoro mingi iliyoanza kujitokeza katika Wilaya hiyo inayowahusisha wakulima na wafugaji.

Katika Mkutano huo wananchi wa Kijiji hicho walililalamikia Jeshi la Polisi katika Wilaya hiyo kwa kutochukua hatua za haraka pale wanapopelekewa taarifa za wafugaji wanaolisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima.

Wakulima hao walisema kuwa wafugaji wanaofanya vitendo hivyo wengi ni wahamiaji katika maeneo hayo na hivyo wamekuwa wakiwasababishia matatizo makubwa ikiwemo kuharibiwa kwa mazao yao na wanapotaka kufanya jitihada za kulinda mazao yao wanaishia kupata kipigo.

Kufuatia malalamiko hayo yaliyotolewa na sehemu kubwa ya wakulima hao, Waziri Ulega alitoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali kuanzia ngazi za chini kuanzisha kamati za usuluhishi ili ziwe zinashughulika na migogoro hiyo mapema kabla haijakuwa mikubwa na kuleta madhara.

Aliongeza pia kwa kulitaka Jeshi la Polisi Wilayani humo kuhakikisha wanatenda haki kwa kila mtu na kwa usawa ili kuondoka lawama zinazowakabili za kuonekana wanawapendelea wafugaji kuliko wakulima.

Vilevile, aliwaekeza watendaji wa wilayani humo kuwa katika kamati hizo watakazoziunda waandae mpango mzuri wa kuweka njia kwa ajili ya kupitishia mifugo ili isiwe inapita katika mashamba ya wakulima.

Aidha, Waziri Ulega alitumia ziara hiyo pia kukemea vitendo vya kujichukulia Sheria mkononi vinavyofanywa na wakulima pamoja na wafugaji akisema kuwa kufanya hivyo ni kosa na ni miongoni mwa vitendo vinavyochangia uvunjifu wa amani.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa katika kuhakikisha maelekezo hayo ya Naibu Waziri yanafanyiwa kazi kwa haraka aliwaagiza Watendaji wake kuhakikisha kamati hizo zinaundwa ndani ya wiki moja.

kuhusu suala la kuweka njia za mifugo, Kawawa alitoa mwezi mmoja kwa wataalam mifugo kwa kushirikiana na wafugaji na wakulima kuhakikisha njia hizo zinawekwa ili kupunguza usumbufu wa mifugo katika mashamba ya wakulima.

Aidha, Mkuu wa Wilaya huyo pia aliwataka wafugaji kuchimba mabwawa ya maji kwa ajili ya mifugo yao na kwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza migogoro ya mara kwa mara na wakulima.

Kabla ya ziara hiyo ya Waziri Ulega Wilayani humo, siku chache zilizopita wafugaji waliuwawa kutokana na migogoro hiyo hiyo ya wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Nanjilinji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akitoa maelekezo kwa Watendaji wa Serikali katika Mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Nakiu Kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi. Ulega alifanya ziara Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero za Wakulima na Wafugaji ambapo baada ya kusikiliza kero hizo  aliagiza kuundwa kwa kamati za maridhiano zitakzaokuwa zinashughulika migogoro hiyo mapema inapojitokeza.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega  akiongea na  wananchi wa Kijiji cha Nanjilinji kwenye mkutano uliofanyika katika Kijiji hicho Kilichopo Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi.  Akiwa katika Mkutano huo aliwasiliana kwa njia ya simu na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji  Tanzania ili aende kujadiliana kwa pamoja wakiwemo wafugaji na viongozi wa Kijiji hicho ili kuzipatia ufumbuzi kero zao.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Zainab Kawawa muda mfupi kabla ya kuanza ziara ya kutembelea Vijiji vya Nakiu na Nanjilinji vilivyopo Wilayani humo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...