MKURUGENZI wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa
Rais, Dkt. Andrew Komba amesema nyenzo kubwa ya kupunguza matumizi ya Zebaki
kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ni kutoa elimu kwa kundi hilo.
Alisema Tanzania ilitekeleza mradi wa kuandaa Mpango kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki ambao ni wa miaka mitano (2020 – 2025) kwa lengo la kupunguza na pale inapowezekana kuondosha matumizi ya kemikali hiyo katika shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu ili kulinda afya ya binadamu na mazingira.
Aidha, Dkt. Komba alisema pamoja na kuwa na lengo kuu la kupunguza matumizi ya Zebaki vilevile unalenga kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala ili kupunguza changamoto za afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.
“Uchimbaji huu mdogo wa dhahabu nchini hutumia kemikali ya Zebaki katika kuchenjua dhahabu. Pamoja na faida kubwa inayopatikana kutokana na sekta hii, shughuli hizi zimekuwa na changamoto kubwa katika afya ya binadamu na mazingira ikiwa ni pamoja na umwagaji maji yenye sumu kwenye mazingira, uchafuzi wa hewa unaotokana na uchomaji holela wa dhahabu, uchenjuaji wa dhahabu usiotumia vifaa kinga, ukataji wa miti kwa ajili ya kupata magogo ya kujengea mashimo,” alisema Dkt. Komba.
Mkurugenzi huyo alisema tafiti mbalimbali zimeendelea kufanyika na kubainisha kuwa Zebaki ni chanzo kimojawapo cha uchafuzi wa mazingira duniani ambapo huchangia takriban asilimia 38 ya uchafuzi wa mazingira na hali inaambatana na athari katika afya ya binadamu.
Aidha, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Zebaki inatajwa kuwa ni miongoni mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya ya binadamu hivyo kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya kimataifa ilipitisha Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki mwaka 2013 wenye madhumuni ya kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara ya uchafuzi wa mazingira unotokana na Zebaki.
Hivyo,
Mpango Kazi huo umeainisha pamoja na mambo mengine Hali ya Sekta ya Wachimbaji Wadogo nchini ilivyo; Malengo
na Shabaha Muhimu ya Mpango–Kazi;
Mikakati ya Utekelezaji ikihusisha Gharama na Utaratibu wa Utekelezaji;
na Uratibu wa Tathmini na Ufuatiliaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...