CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesifu msimamo imara na thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kujali na kuwasikiliza wananchi kwa kushughulikia malalamiko yaliyotokana na makato makubwa kwenye miamala ya simu.
Pia kimesema punguzo la tozo hizo litaleta unafuu kwa wananchi ambao wengi wamekuwa wakitumia miamala ya simu kuendesha shughuli za kiuchumi na kusaidia wahitaji.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka katika ofisi ndogo Lumumba wakati akizungumza na vijana wa taasisi ya Mama yangu , Nchi yangu ambao wanafanya shughuli za kuhamasisha vijana katika uwajibikaji, uzalendo na ubunifu mikakati ya kuwasaidia wanawake na vijana.
Amesema uamuzi wa serikali umetolewa wakati muafaka ingawaje akasisitiza wananchi bado wana wajibu wa moja kwa moja kuchangia maendeleo ya Taifa.
Shaka amesema kitendo kilichofanywa na serikali ya Rais Samia ni cha kizalendo kwa kuwajali wananchi wake na kwamba ameonesha uungwana wa kiwango cha juu kusikiliza kilio cha wananchi na kutekeleza matakwa yao.
"CCM inampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwasikiliza wananchi kuhusu sakata la tozo za miamala ya simu ambapo alitoa maelekezo ya viwango hivyo kutazamwa upya na sasa imepunguzwa kwa asilimia 30 huku makampuni yakipunguza kwa asilimia 10. Kazi ya kujenga nchi ni wajibu wa watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa. Uamuzi huu ni upendo mkubwa alionao kwa wananchi anaowaongoza ili washiriki kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa furaha,"amesema Shaka.
Amefahamisha kuwa hata hivyo kila mwananchi anatakiwa kuelewa kazi ya ujenzi wa nchi, kuweka msukuko wa maendeleo na shime ya upelekaji huduma za jamii katika maeneo yote ni kazi na jukumu la kila mwananchi kwani serikali ni watu na watu ndiyo wananchi wenyewe.
Pia Shaka aliwataka watendaji wote dhamana kuelewa kuwa kazi ya kumsadia Rais katika kila eneo ni wajibu usiohitaji kuelelezwa wala kusukumwa badala yake kila mmoja atimize wajibu wake ipasavyo wakiweka mbele maslahi ya umma.
Hata hivyo katibu mwenezi huyo Shaka aliwataka watanzania kupuuza uvumi unaoenezwa mitaani kuwa serikali ina mpango wa kusitisha elimu bila ada.
"Serikali ya Rais Samia itaendelea kugharamia elimu bila ada kwani unawagusa na kuwanufaisha wananchi walio wengi. Zaidi itaendelea kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili mpango huu ili wanafunzi wakitanzania wapate elimu katika mazingira mazuri zaidi. Hivyo niwaombe wananchi wapuuze taarifa zinazodai serikali itausitisha." amesema Shaka.
Mwenyekiti wa kundi hilo Agness Maganga ameeleza wanampongeza na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu serikali anayoiongoza imefanya mambo makubwa ikiwemo kupandisha madaraja watumishi wa umma 92000, kuondoa tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya mkopo kwa wanufaika wa mkopo elimu ya juu, kuongeza bajeti ya mikopo elimu ya juu na kuendelea kutoa fedha kukamilisha na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati kiuchumi nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...