Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 15 Septemba, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Sudan ya Kusini Salva Kiir Mayardit, Balozi Albino Ayuel Aboug, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Balozi Aboug amesema ujumbe huo pamoja na mambo mengine, Mhe. Rais Salva Kiir Mayardit ametaka kuimarishwa zaidi kwa uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Sudan Kusini.
Amesema Sudan Kusini inaomba kutumia Bandari ya Dar es Salaam kusafirisha mizigo yake na pia kununua chakula kutoka Tanzania.
Aidha, Balozi Aboug amesema Sudan Kusini pindi Reli ya Kisasa (SGR) itakapokamilika ingependa kusafirishia bidhaa zake kupitia reli hiyo.
Pia, amesema Sudan Kusini bado inahitaji kupata walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili kuanzia ngazi ya shule za msingi kutoka nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amemuhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano na uhusiano uliopo kwa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kuhusu ombi la kutumia Bandari ya Dar es Salaam, Mhe. Rais Samia amemuhakikishia mjumbe huyo kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Sudan Kusini kutumia Bandari ya Dar es Salaam katika kukuza uchumi wa nchi zote mbili.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...