Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
Timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imefanikiwa kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mchezo uliopigwa kwenye dimba la Stade de TP Mazembe mjini Lubumbashi ikiwa ni mchezo wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022 Michuano itakayofanyika nchini Qatar.
Taifa Stars iliyo katika nafasi ya 135 katika viwango vya Soka ulimwenguni ikiwa chini ya Kocha Kim Paulsen, bila ya Nahodha wake Mbwana Ally Samatta ilifanikiwa kupata sare hiyo mbele ya timu bora ya DR Congo inayoshika nafasi ya 65 katika viwango vya Soka ulimwenguni, iliyo sheheni idadi kubwa na jopo la Wachezaji wanaocheza Soka la kulipwa nje ya taifa hilo.
Katika mchezo huo, DR Congo dakika ya 23 walianza kupata bao kupitia kwa Mshambuliaji wake, Dieumerci Mbokani anayecheza katika Klabu ya Kuwait SC ya nchini Kuwait, wakati bao la kusawazisha la Tanzania likifungwa maridadi na Mshambuliaji Simon Msuva anayecheza katika Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, katika dakika ya 35 ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo.
Kwa matokeo hayo Taifa Stars na DR Congo wanagawana alama moja katika msimamo wa Kundi J la kuwania kufuzu Michuano hiyo ya Kombe la Dunia nchini Qatar, wakati ikiwa ni faida kwa Tanzania kupata sare hiyo ugenini huku ikiwasubiri Madagascar Septemba 7, 2021 katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Taifa Stars ilifanya mabadiliko kadhaa ili kuwa bora na kuwazuia DR Congo, dakika ya 57 kipindi cha pili iliwatoa Dickson Jon na kuingia Bakari Nondo Mwamnyeto, ikimtoa pia Novatus Dismas na kuingia Mudathir Yahya Abbas.
DR Congo wao waliwatoa, Alaba Akolo, Mbokani na kuwaingiza Luamba Ngoma na Ngita Ben Malango katika kipindi cha pili cha mchezo huo.
Kundi J la Michuano hiyo linajumuisha timu za taifa za Tanzania, DR Congo, Madagascar na Benin.
Mchezo wa pili utakaopigwa nchini Tanzania Septemba 7 mwaka huu Taifa Stars inategemewa kuwa na Nahodha wake, Mbwana Samatta ambaye katika mchezo dhidi ya DR Congo alichelewa kutokana na kumalizia usajili wake katika timu yake mpya ya Royal Antwerp FC ya Ubelgiji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...