Na Amiri Kilagalila,Mahanje
Wananchi
wa kijiji cha Mahanje kilichopo halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani
Ruvuma wapo hatarini kuugua kutokana na maji wanayotumia kuwekwa dawa na
baadhi ya wakulima wanaolima mazao katika vyanzo vya maji.
Aidha
wananchi wa kijiji hicho pia wanaweza kukosa kabisa maji hapo mbeleni
kutokana na kukauka maji hali inayosababishwa na Kilimo kinachoendelea
karibu na vyanzo vya maji pamoja na ukataji wa miti hovyo.
Hayo
waliyasema kijijini hapo na wananchi wakati wakizungumza na waandishi
wa habari kuelezea kero hiyo ambayo imechukua muda mrefu pasipo kupata
utatuzi.
Walisema kwenye
kijiji hicho kuna vyanzo viwili tu vya maji ambavyo vimeharibiwa na
baadhi ya wakulima wanaofanya shughuli za binadamu katika milima na
kupelekea uharibu wa vyanzo hivyo vya maji.
Walisema
maji wanayokunywa kwasasa yana dawa ambazo wakati wa kunyunyiza kwenye
mazao zimekuwa zikienda kwenye vyanzo vya maji ambayo wananchi hao
wanayatumia.
Walisema
licha ya juhudi za viongozi wa serikali katika kuzuia shughuli za
binadamu katika vyanzo vya maji lakini wakulima hao wamekuwa wakikahidi
maagizo hayo.
Walisema
baadhi ya wafugaji kutoka kijiji cha Matetereka wamekuwa wakichunga
katika maeneo ya vyanzo vya maji na kusababisha uchafuzi wa maji hayo.
Baadhi
ya wananchi hao wakiwemo Vestina Ngatunga, Gerlod Mwenda na Uric
Kinyero walisema zaidi ya miaka mitatu wamekuwa wakifanya jitihada
mbalimbali za kuondoa tatizo hilo lakini mpaka sasa muafaka
haujapatikana.
Walisema
kuendelea kwa shughuli za binadamu kwenye vyanzo hivyo vya maji ikiwemo
ukataji wa miti unasababisha kupungua kwa kiwango cha maji kwenye vyanzo
hivyo.
"Mwaka 2019
tulienda kwenye vyanzo vya maji tukakuta wakulima wanalima maharage na
kutumia dawa ili kuulia zile nyasi tulichukua maji kwenye chupa na
kuyaleta kwa viongozi wa kijiji ili kuona kama yanafaa kwa matumizi ya
binadamu" alisema Uric.
Mwenyekiti
wa watumia maji wa kijiji cha Mahanje Adelat Kilewa alisema tatizo hilo
la wananchi kunywa maji machafu ni la muda mrefu tangu hajaingia
madarakani lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu kwenye kutatua tatizo
hilo.
Alisema viongozi wa serikali wamekuwa wavivu katika kutatua matatizo ambayo wananchi yanawakabili.
Alisema
wakati wa ziara ya mbunge wa jimbo hilo la Madaba Joseph Mhagama
wananchi walitoa kero hiyo huku wakimuonyesha maji kwenye kopo ambayo
hayastahili kwa matumizi ya binadamu.
"Maji
yanapatikana kwa kusuasua na machafu zaidi Hawa wenzetu wa milimani
wanapiga dawa na najua baada ya muda wananchi hawa ambao ni watumia maji
watapata kansa" alisema Kilewa.
Mtendaji
wa kijiji cha Mahanje Jabir Fuse alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya
kuchafuliwa kwa vyanzo vya maji ambapo hatua alizochukua Ni kuwakamata
wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wanafanya shughuli za binadamu katika
vyanzo vya maji.
Alisema
shida kubwa inayofanya vyanzo hivyo vya maji kuchafuka ni wakulima
ambao wamekuwa wakilima vinyungu na kusababisha kuchafuka kwa maji hayo.
"Changamoto
iliyopo katika vyanzo hivyo vya maji kuna sehemu ya mipaka katika
kijiji cha Mahanje na Matetereka ambacho hakipo katika eneo la utawala
wangu" alisema Fuse.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...