WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo amefanya ziara kwenye Mto Mbezi na Msimbazi kukagua namna utekelezaji wa muongozo wa usafishaji mito Mkoa wa Dar es Salaam uliotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na kubaini kuwa unafuatwa.
Akiongea kwenye ziara hiyo Waziri Jafo amekipongeza kikosi
kazi kinachosimamia muongozo huo ambacho kinajumuisha Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam pamoja na Halmashauri zote za Wilaya
za Mkoa wa Dar es Salaam.
"Nakipongeza kikosi kazi kwa kazi kubwa ya kulinda
mazingira yetu, kinahakikisha masharti
yaliyotolewa kwenye vibali vya kusafisha mito yanafuatwa na mpaka sasa ni
takribani kilometa 47 zimeshasafishwa" amesema Mhe. Jafo
Mhe. Jafo ameongeza kuwa ukifuatwa utaratibu mzuri wa
kusafisha mito kama muongozo unavyotaka itasaidia kuepuka uharibifu wa kingo za
mito jambo ambalo linasababisha kuhama kwa mtiririko wa maji ya mto katika asili yake na kuleta
mafuriko.
Katika hatua nyingine Mhe. Jafo amepiga marufuku kwa mtu
yeyote kuchimba mchanga bila kufuata utaratibu uliowekwa wa kusafisha mito.
" Hatua kali za Kisheria zitachukuliwa kwa mtu yeyote
atakayebainika anachimba mchanga bila
kibali cha bonde au mamlaka husika".
Aidha Mhe. Jafo amewataka Wakandarasi wote wanaofanya
shughuli za usafishaji mito wafanye kazi kwa weledi na wazingatie masharti
yaliyowekwa na Serikali.
Naye Kaimu Mkurugenzi (Kurugenzi inayosimamia utekelezaji na
usimamiaji wa Sheria ya mazingira) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi (NEMC) Mhandisi Redemta Samwel amesema Sheria ya Mazingira ni suala
mtambuka, linaanzia kwenye ngazi ya Taifa mpaka kwenye familia kwahiyo kila
mmoja anawajibika katika utunzaji wa mazingira.
Ameongeza kuwa uchimbaji wa mchanga holela kwenye mito ni kosa kwa
mujibu wa Sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli zozote za kudumu
kwenye vyanzo vya maji ndani ya mita 60.
"Sheria ya Mazingira inazuia kufanya shughuli za kudumu
ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji, hivyo kuchimba mchanga bila kuwa na
utaratibu na kibali maalumu ni kuvunja Sheria ya Mazingira".
Naye Dkt. Elizabeth Mshote Kaimu Mwenyekiti wa kikosi kazi
cha usimamizi wa usafishaji mito amesema
shughuli ya usafishaji mito unaenda sambamba na utunzaji wa kingo,
kuondoa taka ngumu na tope ndani ya mito na jambo hili linaendea kufanywa
vizuri na Wakandarasi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...