Na Said Mwishehe, Michuzi TV
KITUO cha Utamaduni cha Alliance Francaise jijini Dar es Salaam kwa kushirikana na wadau wengine kinatarajia kuwakutanisha wasanii zaidi ya 128 kupitia tamasha la Marafiki linatarajia kuanza Oktoba 7 hadi 10,2021.
Kwa mujibu wa ratiba , Oktoba 7 na Oktoba 8 litafanyika Nafasi Art Space Mikocheni, Oktoba 9 litafanyika Kituo cha Alliance Francaise ambacho kipo chini ya Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania na Oktoba 10 tamasha litafanyika Firefly -Bagamoyo.
Akizungumza wakati kutangaza tamasha hilo leo Oktoba 5,2021 ,Mkurugenzi wa Alliance Frabcaise Flora Valleur amesema Marafiki ni tamasha la muziki la kimataifa ambalo huwaleta wasanii wa ndani na wa nje kuonesha umahiri wao katika eneo la sanaa ya muziki.
"Tamasha hili linaleta wadau na watalaam wa sanaa kushiriki pamoja na kubadilishana uzoefu na maarifa kwa lengo la kuwajengea uwezo wasanii katika maeneo mbalimbali ya sanaa.Tamasha la Marafiki linatarajia kuleta muziki mzuri wa moja wa moja na maarifa wakati mmoja kuanzia Oktoba 7 hadi Oktoba 9,'amesema Valleur.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tamasha la Marafiki, Isack Kabeneko amesema wametangaza rasmi tarehe za kufanyika kwa tamasha hilo na tiketi zitanza kuuzwa mapema kwa Sh.10,000 na watakaonunua mlango Sh.15,000.Tiketi zinapatikana Nafasi Art Space -Mikocheni, Firefly -Bagamoyo na Alliance Francaise-Dar es Salaam,"amesema.
Akifafanua kuhusu tamasha hilo amesema kauli mbiu ya mwaka hii inasema "Muziki ni kwa maendeleo ya kijamii", hivyo wamejikita kuhamasisha vijana ambao wamejiajiri kupitia sanaa kutengeneza tungo zenye tija na maudhui kwa jamii na kugusia maeneo tofauti tofauti.
"Katika tamasha la Marafiki tutakuwa na wasanii 128, bendi 16 na wote watatumbuiza wakati wote wa tamasha likiendelea katika maeneo ambayo tumetaja, wasanii wataonesha vipaji vyao katika kuimba na sanaa nyingine tofauti tofauti.Kwa kutambua ukubwa wa tamasha hilo mbali ya wasanii kuonesha umahiri wao katika eneo la sanaa.
"Tutakuwa na semina za mafunzo na mijadala ya wazi, lengo ni kundeleza sekta ya sanaa kwa kuweka mipango ambayo tunaamini wasanii watanufaika kupitia sanaa wanayoifanya.Mafunzo yatajikita kuwajengea uwezo wasanii,"amesema.
Amefafanua wanataka kuona jamii ya wasanii yenye maendeleo , yenye tija na kunufaika kupitia sanaa huku akieleza kuwa kupitia tamasha hilo wanawake watakuwa na fursa ya kupaza sauti zao kuelezea wanachotaka ili mambo yaende.
Kwa upande wake Ibrahim Ibengwe kutoka Baraza la Sanaa Tanzania(BASATA) amesema baraza hilo linafurahishwa na jitihada ambazo zinachukuliwa na wadau wa sanaa katika kuendeleza sekta hiyo.Hivyo wamekuwa wakiunga mkono wadau wote ambao wanaweka mikakati ya kuiendeleza sekta ya sanaa nchini.
"BASATA tumekuja hapa Alliance Francaise kwa ajili ya kuwaunga mkono wadau wetu muhimu katika sekta ya sanaa nchini kwa maana ya wandaaji wa matukio mbalimbali ya sanaa, hivyo Marafiki Festival ni miongoni mwa matukio yanayoratibiwa na baraza letu.
"Kwa hiyo tunaendelea kutekeleza juhudi za Serikali kwa kuhakikisha shughuli za sanaa hasa matamasha yanafanyika kwa ubora stahiki, kuna vigezo ambavyo BASATA tunavizingatia kuhakikisha matukio haya yanafanyika kwa taratibu unaoeleweka ili yawe na tija kwa Serikali, wasanii na waandaaji,"amesema Ibengwe.
Ameongeza lengo la matamasha hayo ni kutengeneza mazingira rafiki na kutoa fursa kwa wadau wa sanaa, kwa maana wasanii wa aina zote kuonesha kazi zao kupitia tukio hilo na wanapozionesha watalipwa, hivyo wataogeza kipato.Pia kutakuwa na shughuli nyingine za kijamii ambazo kupitia shughuli hizo jamii nayo itapata fedha.
Baadhi ya wasanii watakaoshiriki kwenye tamasha hilo ni Akoth Jumadi, Bahati Female Band, Balaa MC,Dabo Mtanzania, Iju Music, Justine Kaozya, Kudra Mazongela, Nasibo Mutize, Sinaubi Zawose na Stone Town Rockerz.
Wengine ni Tarajazz Zanzibar, Tofa Boy, Voice Revolution Band, Witiri Ubuntu na Ziad Daroueche.Tamasha litakuwa linaanza saa 12 jioni hadi saa sita usiku wakati semina ya mafunzo na mijadala itakuwa inafanyia kuanzia saa nne asubuhi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...