Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajloui ( wa nne kushoto) akiwa na Vijana wa Kitanzania waliopata mualiko wa Serikali ya Ufaransa kuhudhiria mkutano mkubwa uliotishwa na Rais wa nchi hiyo kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali kati ya nchi yao na nchi za Bara la Afrika
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui(kulia) akizungumza na waandishi wa habari mbele ya baadhi ya Watanzania waliopata mualiko wa kuhudhuria mkutano mkubwa uliondaliwa na Rais wa Ufaransa Emmaneul Macron utakaofanyika katika Jiji la Paris, mkutano unahusisha nchi ya Ufaransa na nchi za Afrika.
Mwandishi wa Habari la Shirika la Ufaransa na mchora katuni Jumanne Mohamed maarufu Meddy( kushoto) akiwa na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajloui( kulia) akikabidhi mchoro wa picha kwa balozi huyo.
Balozi wa Ufaransa nchin Tanzania Nabil Hajloui( kushoto) akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu mkutano mkubwa unaotarajia kufanyika Paris nchini Ufaransa
Sehemu ya watanzania waliopata mualiko wa Serikali ya Ufaransa wakiwa Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania wakati Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania akizungumzia mkutano mkubwa utakaofanyika katika Jiji la Paris.
Matukio mbalimbali katika picha wakati Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajloui alipokutana na waandishi wa habari kuhusu mkutano mkubwa utakaofanyika nchini Ufaransa Oktoba 8 mwaka huu.Mkutano huo unalenga nchi ya Ufaransa kufufua uhusiano mpya na nchi za Afrika
Na Said Mwishehe,Michuzi TV
BALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui amekutana na baadhi ya vijana wa Tanzania watakaoshiriki mkutano mkubwa uliondaliwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika Jiji la Paris kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya kibiashara,uchumi ,usawa wa kijinsia kati ya nchi hiyo na Bara la Afrika.
Akizungumza leo Oktoba 1,2021 ,katika Ofisi za Ubalozi wa Ufaransa nchini, Balozi Hajlaoui amesema Oktoba 8 mwaka huu kutakuwa na mkutano mkubwa katika nchi yao na dhima ya kuandaliwa kwa mkutano na Rais ...ni kuonesha mchango wa nchi yao kwa Tanzania,ndi maana wamechukua vijana 14 wa Tanzania kushiriki mkutano huo.
Miongoni mwa vijana hao kutoka kampuni, taasisi, mashirika, wajasiriamali na wafanyabiashara yupo pia Mwandishi wa habari na Mchora Katuni Jumanne Mohamed maarufu Meddy ambaye anafanya kazi Shirika la Utangazaji la Ufaransa.
Balozi Hajloui amesema vijana hao watashiriki na kwenda kuchangia maoni yao mbele ya Rais wa Ufaransa ambaye atawapa fursa ya kuwasililiza zaidi na kwamba wadau wote watakaohudhuria mkutano watakuwa na maoni yatakayosaidia kujenga,kuboresha na kufufua mahusiano mapya kati ya Ufaransa na Afrika.
Pia kupitia mkutano huo wataangalia namna bora za kutatua changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi lakini pia kujadili kwa kina usawa wa kijinsia."Mkutano huo mkubwa ni matarajio yetu utaleta utatuzi wa changamoto mbalimbali,"amesema.
Kwa upande Wake Ofisa wa Mauzo ya Chakula kutoka Bakharesa Group Ltd Salum Azizi amesema kwamba wanatoa shukrani kwa Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kwa kuamua kuwapa nafasi ya kwenda kushiriki Mkutano mkubwa ulioandaliwa na Rais wa Ufaransa wenye lengo la kujadili kwa kina masuala mbalimbali kama mwanzo wa ujenzi wa uhusiano mpya kati ya Ufaransa na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
" Mkutano huo lengo lake hasa ni kufanya majadiliano na kuangalia fursa za kibiashara,hivyo Bakharesa Group tunatoa shukrani za dhati wa Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania ,kwa kututambua na kuwa sehemu ya washiriki tutaokwenda kwenye mkutano huo.
"Kwa hiyo tunathamini heshima hii ambayo tumeipata,nasi tunaahidi tutarejesha thamani hiyo kwa vitendo, tunafanyabiashara katika nchi mbalimbali duniani,hivyo hii kwetu ni fursa,"amesema.
Aidha amesema watahakikisha wanaiwakilisha vizuri nchi ya Tanzania katika mkutano huo hasa kwa kutambua kwenye sekta binafsi nchi yetu imejipanga vizuri na kampuni ya Bakharesa ni moja ya kampuni kubwa inayofanya vizuri, kwani inafanya biashara na mataifa mengine makubwa kama Ufaransa na Ujeruman na wanatambulika kama kampuni kubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiave Rebeca Gyumi amesema Serikali ya Ufaransa na Rais wake kwa kutoa mualiko kwa Watanzania kushiriki mkutano huo mkubwa na hasa kwa kuangalia nchi ya Ufaransa inavyoimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika.
Amesema kwao kama vijana wa Tanzania ni nafasi muhimu ya kupeleka habari njema kwa yale yanayoendelea nchini hususani jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali ya kupeleka ujumbe wa usawa wa kijinsia.
"Tunaamini hii ni fursa kwetu na tunapokwenda tunajua tutarudi na ujumbe maalum wa muelekeo wa Ufaransa katika kushirikiana na Tanzania kuleta maendeleo endelevu kwa manufaa ya nchi yetu.Kwa hiyo safari yetu kwenye mkutano huo utakaofanyika Oktoba 8 unakwenda kuonesha picha halisi ya kile ambacho kama nchi tutanufaika nacho,"amesema Gyumi.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Kampuni ya Atsoko ambayo inajihusisha na uletaji na usambazaji wa bidhaa za vipodozi Rehema Julius amesema anashukuru kupata fursa ya kwenda kuwawakilisha wenzake nchini Ufaransa na safari hiyo inamaana kubwa kwa kampuni yake kwani kuna changamoto kubwa ya kupata bidhaa zenye viwango kwani bidhaa nyingi zinaharibu ngozi wa watumiaji hasa wanawake na vijana .
Hivyo kupata fursa ya kwenda kushiriki mkutano ulioandaliwa na Rais wa Ufaransa utamuwesesha kukutana na wazalishaji wa bidhaa hizo na watapata kujifunza kutoa kwao."Tutazungumzia ushirikiano wa kibiashara na tutakuwa tayari kununua bidhaa kutoka nchi hiyo na hivyo tutakuwa na uhakika wa ubora wa bidhaa zinazoingia nchini kwetu,"amesema
Aidha amesema inasikitisha kuona bidhaa zenye ubora duni zikiendelea kuingia nchini kupitia njia za panya,hivyo ameishauri Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania( TBS) kuimarisha udhibiti wa uingizaji bidhaa ambazo ziko chini ya ubora."TBS waongeze udhibiti mipakani na njia za panya,zinapoachwa na kuingia madhara yake ni makubwa."
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...