Mratibu wa Shirika lisilo la kiserikali la FEET Tanzania Alfred Kiwuyo (watatu kushoto) akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 11 , 2021 wakati wa uzinduzi wa Mradi wa STEM unaolenga kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.Mradi huo ambao umezinduliwa leo utakwenda hadi Desemba 11 mwaka huu ambao kutakuwa na shindano kwa muda wote na washindi watapewa zawadi.Wengine katika picha hiyo ni wanafunzi wa shule za sekondari ambao wameshiriki tukio hilo.
Mwanafunzi wa kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Temeke,Dar es Salaam Ahlam Hamad(katikati) akizungumza kuhusu umuhimu wa Mradi wa STEM ambao umezinduliwa na FEET Tanzania kwa lengo la kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.Kushoto ni Mratibu wa FEET Tanzania Alfred Kiwuyo na kulia ni Noela Massawe ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Temeke.
Mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Juhudi Said Rajab (katikati) akizngumza kuhusu mradi huo ambapo ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha wanafunzi wa kike kupenda masomo ya sayansi, kwani sio magumu.Kulia ni Mratibu wa FEET Tanzania Alfred Kiwuyo na kushoto ni mwanafunzi wa Sekondari ya Temeke Ahlam Hamad.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Temeke Donatila Thomas(katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mradi wa STEM wenye lengo la kuhamasha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.
Said Rajab ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Juhudi (watatu kulia) akifafanua jambo baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa
mradi wa STEM unaolenga kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.
Mwanafunzi wa kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Temeke,Dar es Salaam Ahlam Hamad(wapili kushoto)akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi.
Mratibu wa FEET Tanzania Alfred Kiwuyo( watatu kulia) akifafanua jambo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa STEM.


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

TAASISI ya FEET Tanzania imezindua Mradi maalumu uliopewa jina la STEM kwa lengo la kuhamasisha watoto wa kike walioko katika Shule za Sekondari nchini kupenda masomo ya sayansi huku ikieleza kupitia mradi huo shule za sekondari 100 zitashindana kupata wanafunzi wa kike watakaokuwa na mawazo na maoni mapana kuhusu masomo ya sayansi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam ,Mratibu wa FEET Tanzania Alfred Kiwuyo amesema leo Oktoba 11 , 2021 ni siku ya Mtoto wa Kike Duniani, hivyo taasisi yao ambayo siyo ya kiserikali imeamua kuzindua mradi huo ambao utakwenda hadi Desemba 11 mwaka huu na kisha kumalizika kwa tukio kubwa la kutoa zawadi kwa sekondari bora na wanafunzi bora katika masomo ya sayansi.

''FEET Tanzania tumejikita katika kusaidia elimu kwa mtoto wa kike , usawa wa kijinsia pamoja na kuuhisha ushiriki wa vijana katika masuala ya mazingira.Nia yetu kubwa ni kuboresha mazingira rafiki ya mtoto wa kike kwenye jamii, pamoja na kuzingatia usawa katika elimu.

''Leo Oktoba 11 tuko hapa kuzindua programu ya STEM inayohusu watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi, tumegundua katika masomo ya sayansi watoto wa kike wameachwa nyuma sana, hata katika ripoti ya BEST mwaka 2016 inaoesha ufaulu wa watoto kike kwenye masomo ya sayansi umekuwa mdogo , pia uelewa wao umekuwa mdogo, hivyo tumeona tuje na mradi huu wa kuhuhisha masomo ya sayansi ili mtoto wa kike apende kusoma, pia kuangalia namna gani tunaweza kuongoza ufauli wa mtoto wa kike katika masomo ya sayansi,'' amesema.

Amefafanua mradi huo wa STEM umejikita katika masuala sayansi, teknolojia , Uhandisi na hesabu na lengo ni kumsaidia mtoto wa kike.

''Mradi huu unakwenda kumfanya mtoto wa kike kuwa karibu na kupenda zaidi masomo ya sayansi kwa kubuni project ambazo zitakuwa na tija, Tumezindua mradi huu leo Oktoba 11 na itakwenda mpaka Desemba 11 ambapo wanafunzi wa kike watatengeneza project za kisayansi, mawazo mapana katika sayansi, na tutatoa zawadi kwa shule bora na watoto bora wa kike watakaokuwa wameleta mawazo mazuri ya kisayansi watazawadia vifaa vya maabara na vitabu vya masomo ya sayansi, lengo ni watoto wa kike kupenda sayansi, amesema.''

Kiwuyo amesema kauli mbiu ya Siku ya Mtoto wa kike inaweka wazi namna ya kumsaidia mtoto wa kike kupenda masomo ya sayansi na katika kuuhisha teknolojia kwa mtoto wa kike, hivyo FEET wameona waje na mradi huo.

Kwa upande wake Mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Temeke anayechukua mchepua wa masomo ya sayansi Ahlam Hamad amesema FEET Tanzania wamefanya jambo kubwa kuja na mradi huo na wanaamini utakwenda kuongeza chachu wanafunzi wa kike kupenda masomo ya sayansi.

''Watoto wa kike tumekuwa nyuma sana kuingia katika miradi inayohusu sayansi , kwasababu tofauti tofauti ikiwemo ya kutokuwepo kwa muongozo ambao unahusu watoto wa kike , kuna changamoto ya uhaba wa walimu wa sayansi,'' amesema.

Wakati huo huo Mwanafunzi wa Shule ya sekondari Temeke Noela Massawe ametoa ombi kwa Serikali kama kuna uwezekano iweke mikakati ya kuanzisha programu za kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya sayansi, pia iongeze walimu ambao watasaidia watoto wa kike kusoma sayansi.

''Sio watoto wote wa kike hawapendi kusoma sayansi bali wakati mwingine kuna changamoto zinazosababisha kushidwa kusoma, kwa mfano unakuta mtoto wa kike anapenda kusoma sayansi lakini mazingira ya nyumbani yanamkwamisha.''

Kwa upande Mwanafunzi Donatila Thomas wa kidato cha tano sekondari ya Temeke amesema anawashauri wanafunzi wa kike kupenda masomo ya sayansi kwani ni mazuri na yana ajira zinazoeleweka na kwamba Serikali inatoa kipaumbele zaidi kwa watoto wa kike wanaopenda sayansi.

''Masomo ya sayansi yana ajira nyingi, watoto wa kike wasome kwa bidii kwani hata Serikali inatoa kipaumbele, hivyo niwatoe hofu wanafunzi wa kike kuhusu msomo ya sayansi, ni masomo ya kawaida na sio magumu kama ambavyo wengi wamekuwa wakituminisha, kikubwa tujiamini na tunaweza,'' amesema.

Mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Juhudi Rajab amesema wameamua kuungana na FEET Tanzania kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa mradi wenye nia njema na mtoto wa kike kuhakikisha anapenda masomo ya sayansi."Ushauri wangu kwa watoto wa kike wajitahidi kusoma masomo ya sayansi na sio tu kwa ajili ya kujinufaisha wa o peke yao bali wanufaishe na jamii kwa ujumla,"amesema Rajabu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...