Afisa Utawi wa Jamii katika Jiji la Dodoma, Heriely Kutwama akitoa elimu kwa kundi la watoto waliotembelea banda la Idara ya Afya

Na Dennis Gondwe, Chinangali Park-DODOMA
JAMII imetakiwa kutoa kipaumbele kwa masuala ya ulinzi na usalama wa mtoto ili kumuepusha na ukatili wa kijinsia na kumuhakikishia makuzi bora ili aweze kuwa raia mwema na kutoa mchango wake kwa taifa.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Rebeka Ndaki alipokuwa akielezea umuhimu wa ulinzi na usalam wa mtoto katika jamii kwa wananchi waliotembelea banda la Idara ya Afya la Halmashauri hiyo katika Bustani ya Mapumziko Chinangali jijini Dodoma kwenye maonesho ya Karibu Dodoma Festival.

Ndaki alisema kuwa watoto wote wana haki ya kuishi katika mazingira bora na salama yasiyo na aina yoyote ya vitendo vya ukatili. “Kila mtoto ana haki ya kuishi na kufuraia maisha yake katika jamii kama walivyo watoto wengine. Na mwenye jukumu la kumhakikishia mtoto ulinzi na usalama wake ni jamii nzima inayomzunguka mtoto” alisema Ndaki.

Afisa Ustawi huyo alisema kuwa watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili sana katika jamii. Bahati mbaya jamii nayo imekuwa ni sehemu ya kuuendeleza ukatili huo. Vitendo vivyo vimekuwa vikiwaathiri Watoto kisaikolojia na kimakuzi na kuzuia kutimizwa kwa ndoto zao, alisema. 

“Nitumie nafasi ya maonesho haya ya Karibu Dodoma Festival kuikumbusha jamii kuwa ndiyo mlinzi namba moja wa mtoto. Sisi kama Halmashauri tumeshiriki katika maonesho haya kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu ulinzi na usalama wa mtoto dhidi ya vitendi vya kikatili. Lakini pia tupo hapa kuelezea huduma zinazotolewa na Seksheni ya Ustawi wa Jamii iliyo chini ya Idara ya Afya katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Ndaki.

Aidha, alizitaja huduma zitolewazo na seksheni hiyo kuwa ni elimu ya usajili ya vituo vya kulelea watoto wadogo mchana ‘day care’, elimu ya ukatili wa kijinsia na Watoto na huduma ya familia na malezi. Huduma nyingine alizitaja kuwa ni usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 na huduma ya msaada wa kisaikolojia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...