Charles James, Michuzi TV

WAKATI Jiji la Arusha likiongoza kwenye orodha ya majiji yaliyokusanya mapato mengi kwenye robo ya kwanza ya mwaka wa fedha kwa kukusanya asilimia 27 ya makisio ya mwaka, Jiji la Dodoma ambalo ndio Makao Makuu ya Nchi limekua la mwisho kwa kukusanya asilimia 16 ya makisio yake ya mwaka.

Kwa upande wa Mikoa iliyoongoza kwa ukusanyaji wa mapato, Mkoa wa Manyara umeongoza kwa kufikisha asilimia 40 ya makisio yake ya mwaka huku Mkoa wa Dodoma ukishika mkia kwa kukusanya asilimia 18 ya makisio yake.

Akisoma taarifa ya ukusanyaji wa mapato kwenye Halmashauri 184 nchini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu amesema taarifa hii ya robo ya kwanza ni kipimo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri nchini na kwamba ambao wataendelea kufanya vibaya kwenye halmashauri zao katika taarifa ya robo ya pili basi watapeleka ushauri kwa Mamlaka ya uteuzi (Rais) ili wachukuliwe hatua.

Waziri Ummy amesema anafahamu Wakurugenzi wengi wa Halmashauri ni wageni na kwamba hii ndio taarifa yao ya pili hivyo wakae wakijua kuwa wanapimwa mwenendo wao na taarifa ya robo ya pili itaonesha ni Wakurugenzi wapi ambao hawana kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Akitoa taarifa hiyo, Waziri Ummy amesema katika eneo la Halmashauri za Majiji, Jiji la Arusha ndio limeongoza kwa kukusanya asilimia 27 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Jiji la Dar lililokusanya asilimia 26, Tanga asilimia 25 na Dodoma ikishika mkia kwa kukusanya asilimia 16.

Kwa upande wa Mikoa, Mkoa wa Manyara umeongoza kwa kukusanya asilimia 40, Simiyu asilimia 35 wakati Dodoma ikishika mkia kwa kukusanya asilimia 18 ya makisio yake ya mwaka.

" Kwenye eneo la Halmashauri za Manispaa, kinara wa kundi hili ni Manispaa ya Kahama iliyokusanya asilimia 34 ya makisio yake ya mwaka, Bukoba asilimia 32, Mpanda asilimia 29 wakati Manispaa ya Mtwara ikishika nafasi ya mwisho kwa kukusanya asilimia 15 kwenye kundi hili.

Kwenye kundi la Halmashauri za Miji, kinara ni Halmashauri ya Mji wa Mbulu ambao umekusanya asilimia 44 ya makisio yake ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Kibaha asilimia 43, Tunduma asilimia 39 wakati Halmashauri ya Mji wa Nanyamba imekua ya mwisho kwenye kundi hili ikikusanya asilimia 6," Amesema Waziri Ummy.

Katika kundi la Halmashauri za Wilaya kinara wa kundi hilo ni Halmashauri ya Wilaya ya Hanang ambayo imekusanya asilimia 66, Mlele, Meatu na Ngara wakikusanya asilimia 51 wakati Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba imekua ya mwisho katika kundi hili ikikusanya asilimia 3 ya makisio yake ya mwaka.

Waziri Ummy amesema uchambuzi wa taarifa hiyo ya ukusanyaji mapato katika robo ya kwanza unaonesha kuwa Halmashauri tano zimekusanya kwa asilimia 50 au zaidi ya lengo la mwaka wakati Halmashauri 47 zimekusanya kati ya asilimia 30 hadi 49.

Halmashauri 92 zenyewe zimekusanya kati ya asilimia 20 hadi 29 wakati Halmashauri 37 zimekusanya kati ya asilimia 10 hadi 19 na Halmashauri tatu zimekusanya chini ya asilimia 10 na hiyo ni kwa kuzingatia lengo la mwaka.

Amesema kwa mwaka wa fedha huu wa 2021/22 Halmashauri zote za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji zilipanga kukusanya Sh Bilioni 863.9 kutoka kwenye vyanzo vya ndani.

" Katika kipindi cha Julai 1 hadi Septemba 30, 2021 Halmashauri zimekusanya jumla ya Sh Bilioni 212.7ambayo ni sawa na asilimia 25 ya makisio ya mwaka sawa na asilimia 100 ya lengo la mwaka," Amesema Waziri Ummy.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...