WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha miundombinu ili Watanzania waendeshe shughuli zao kama za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa urahisi na kukuza uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.

 

“…endeleeni kutumia fursa za maendeleo zilizoletwa kupitia fedha za kodi katika kujipatia maendeleo na kukuza uchumi wenu kwani mna Serikali imara, Rais imara na wasaidizi wake wanafanya kazi usiku na mchana kwa ajili yenu.”

 

Ameyasema hayo jana (Jumatatu, Oktoba 25, 2021) baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa (km 53.2) akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali mkoani Lindi.

 

Baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo unaosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa wakala huo usimamie vizuri mradi huo na uhakikishe inajengwa kwa viwango.

 

“TANROADS simamieni vizuri ujenzi wa mradi huu na mhakikishe barabara inajengwa kwa viwango na inakamilika kwa wakati. Mliopata ajira katika mradi huu fanyeni kazi kwa weledi hatutarajii kusikia mtu ameiba nondo wala saruji.”

 

Barabara hiyo inajengwa na kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation ya China kwa gharama za shilingi bilioni 59.28 na imepangwa kukamilika Novemba 2022.

 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi, Rogatus Hussein Mativila alisema hadi kufikia mwezi Septemba mwaka huu ujenzi wa barabara hiyo ulikuwa umefikia asilimia 32.

 

Mhandisi Mativila alitaja kazi zilizofanyika katika mradi huo kuwa ni pamoja na kusafisha eneo la ujenzi, ujenzi wa kitako cha barabara, uinuaji wa tuta kwenye maeneo ya mabonde, ukataji wa maeneo yenye miinuko mikubwa na ujenzi wa makalavati.

 

Kadhalika, Mtendaji Mkuu huyo alitaja barabara za mkoa wa Lindi ambazo Serikali imepanga kuzijenga kwa kiwango cha lami kuwa ni barabara ya Liwale-Nachingwea (km 130) ambayo ipo kwenye hatua ya kufanyiwa upembuzi yakinifu.

 

“Barabara ya Kiranjeranje-Namichiga-Ruangwa yenye urefu wa km 102 na barabara ya Masaninga-Nangukuru-Kilwa Masoko yenye urefu wa km 55 tayari zimeshafanyiwa tayari imeshanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina”

 

Akizungumzia kuhusu barabara ya Nangurukuru-Liwale Mhandisi Mativila alisema mkataba wa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina tayari umeshasainiwa na kazi hiyo inatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...