Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na  Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Mwanza katika utaratibu wake wa kila wiki wa kutoa taarifa za utendaji kazi za Serikali.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akionesha Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo jijini Mwanza, picha rasmi yenye alama muhimu (QR code) ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan inayotakiwa kutumika kwenye ofisi na maeneo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Abubakar Karsan akiuliza swali katika mkutano kati ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa  na Waandishi wa Habari leo jijini Mwanza.

Waandishi wa habari wakiuliza maswali wakati  Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza na  Waandishi wa Habari leo jijini Mwanza katika utaratibu wake wa kila wiki wa kutoa taarifa za utendaji kazi za Serikali.

Baadhi ya waandishi wa habari wakipokea vyeti ikiwa ni pongezi kutoka Klabu ya Waandishi  wa Mkoa wa Mwanza, baada ya kushinda Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) kwa mwaka 2020.

(Picha zote na Immaculate Makilika- Idara ya Habari-MAELEZO, Mwanza)

…………………………………………………………………………………………….

Na Ahmed Sagaff – MAELEZO

Mkoa wa Mwanza umepokea shilingi Bilioni 344 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya wananchi katika kipindi cha miezi sita ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hayo yameelezwa leo jijini Mwanza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema kiasi hicho cha fedha kimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya ujenzi (bilioni 219.1), sekta ya afya (bilioni 15.2), sekta ya elimu (bilioni 38.7), miundombinu ya barabara (bilioni 2.4), usambazaji wa umeme vijijini (bilioni 42.6), miradi ya maji (bilioni 20.4) na mradi wa kusaidia kaya masikini unaotekelezwa na TASAF (bilioni 5.6).

Pamoja na hilo, Msigwa amehabarisha kuwa fedha hizo zitaendeleza ujenzi wa Stendi za Nyamhongolo na Nyegezi, Soko la Kisasa la Mjini, Jengo la Abiria pale kwenye uwanja wa Ndege wa Mwanza,  ujenzi wa MV Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, na Daraja la Kigongo – Busisi lenye urefu wa kilometa 3.2.

“Tumeleta shilingi Bilioni 8.3 kwa ajili ya kujenga hospitali tatu za Wilaya ya Sengerema, Kwimba na Misungwi, kumalizia hospitali mbili za Wilaya ya Buchosa na Ilemela, kujenga vituo vya afya vitano na zahanati 21 na kukarabati na kujenga vituo vya huduma 48, aidha tumeleta shilingi Bilioni 6.4 kwa ajili ya kununua dawa,” amefahamisha Msigwa.

Akifafanua kuhusu shilingi bilioni 38.7 zilizoelekezwa kwenye sekta ya elimu mkoani Mwanza, Msigwa ameeleza kuwa shilingi bilioni 11 zinaimarisha miundombinu ya elimu kwenye shule za msingi na sekondari huku shilingi bilioni nane zikigharamia mradi wa elimu bila malipo.

“Na tunatarajia kuleta shilingi bilioni 19.7 kwa ajili ya kujenga madarasa 985, hizi ni zile fedha za Mpango wa Ustawi wa Jamii tulizopata kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF),” amedokeza Msemaji Mkuu wa Serikali. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...