Na Said Mwishehe,Michuzi TV
BOHORI ya Dawa (MSD) imeanza kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kusambaza dawa nchini baada ya kuwepo kwa malalamiko kwa wananchi kuhusu changamoto ya uhaba wa dawa.
Akizungumza leo Oktoba 12,2021 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa MSD Meja Jenerali Gabriel Saul Mhidze amesema walipokea agizo la Waziri Mkuu kwa unyenyekevu mkubwa na wameanza kutekeleza kwa kupeleka dawa maeneo yote.
"MSD inaendelea na mpango wa usambazaji dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara kama moja ya jukumu lake kwa kasi kubwa ambapo hadi kufikia Oktoba 16 hakutakuwa na kituo cha kutolea huduma za afya nchini chenye uhaba wa bidhaa za afya,"amesema Afande Mhidze.
Amefafanua MSD husambaza dawa kwa kuzingatia mzunguko (ILS),yaani mara nne hadi sita kwa mwaka, lakini kutokana na agizo la Waziri Mkuu, wameamua kupeleka dawa hizo hivi sasa badala ya kusubiri mzunguko kama ilivyokua hapo awali.
Pia amesema kutokana na agizo hilo la Waziri Mkuu, mpaka sasa MSD imeshapokea jumla ya makontena 16 ya dawa zenye thamani ya takribani bilioni 43, ambapo tayari yameshaingia na usambazaji wake umeanza, huku nyingine zikiwa njiani.
"Kwa sasa kanda zote za MSD nchi nzima zinaendelea na usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.Wilaya ambazo tayari zimeanza kupokea dawa hizo ni Uvinza DC yenye vituo vya afya 42, ambapo gari ya Scania yenye tani 10.
"Kigoma MC yenye vituo vya afya 13 gari kubwa ya tani 5.5 na Kigoma DC yenye vituo vya afya 38 Land Cruiser mbili zimeshasili na kushusha dawa,"amesema Meja Jenerali Mhidze na kuongeza katika wilaya ya Kasulu DC vituo vya afya 41.
"Kasulu TC yenye vituo vya afya 15 na Buhigwe DC yenye vituo vya afya 28 tayari magari matano yakiwemo magari mawili makubwa, kila moja yenye kubeba tani 5.5 na Toyota Land Cruiser tatu tayari zimewasilisha dawa".
Ametaja maeneo mengine kuwa ni Lushoto yenye vituo 9, Misenyi na Chato vituo 4, Lindi DC yenye vituo 16 na Hai yenye vituo 24 ambapo magari 13 yameshaondoka na kuwasili katika maeneo hayo, ikiwemo Toyota Land Cruiser 6, gari kubwa ya tani 5.5 zipatazo 3, gari kubwa ya tani 10 na Landcruiser hard top mbili.
"Mbali na usambazaji huo, shehena nyingine za dawa Tani 12 zitawasili nchini alhamisi kupitia uwanja wa ndege, huku Oktoba 16 shehena yenye Tani 12 ikitarajiwa kuingia na makontena 18 yenye dawa yanatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote kuanzia kesho kutwa.
"Dawa hizo zipo zitakazowasili nchini kwa kutumia ndege na bahari, lengo likiwa ni kumaliza tatizo la uhaba wa dawa lililojitokeza.Dawa hizo zinazowasili nchini, zinazingatia taratibu zote za manunuzi na ukaguzi na baada ya taratibu za kitaalamu kukamilika zitawafikia wananchi,"amesema.
Amesisitiza MSD haina changamoto ya usafiri kutokana na magari mengi yaliyopo, hivyo dawa hizo zinazoendelea kuwasili zitasafirishwa kwa wakati ili kumaliza changamoto iliyojitokeza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...