Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imewataka Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) nchini kuanzisha vikundi vinavyotokana na kaya maskini ili viweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 ambayo imekua ikitolewa na Halmashauri zote nchini kwa Wanawake, Vijana na Walemavu.

Agizo Hilo limetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora wakati akizungumza na Waratibu wa TASAF Mkoa wa Ruvuma ambapo amewapa mwezi mmoja kuhakikisha kila mmoja anaanzisha vikundi viwili vinavyotokana na Mfuko huo.

Ndejembi amesema mradi wa TASAF ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo inagusa maisha ya watanzania wote wanaotokana na kaya hizo maskini hivyo ni vema waratibu hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuongeza ubunifu ili waweze kuzinyanyua kaya hizo.

Amesema katika kuonesha kwamba serikali inauthamini Mfuko huo katika bajeti ya mwaka huu imepanga kuzifikia kaya zote maskini ambapo kila Kijiji kitaguswa Nchi nzima.

" Huu mradi ni mkubwa ambao serikali yetu inautazama na tena mwaka huu tumeongeza maeneo katika kipindi hiki cha awamu ya Sita kinaanza ambapo hakuna kijiji wala kata itaachwa, kote huko tumelenga kuwafikia walengwa wa TASAF ili waweze kunufaika na fedha zinazotolewa na serikali yako.

Katika kaya wengi wanaojitokeza kupokea fedha ni akina Mama lakini nao wana vijana ambao wanalalamika hawana ajira kati yenu nani ameanzisha kikundi kinachotokana na TASAF ili waweze kunufaika na ile asilimia 10 ya fedha za Halmashauri? Hivyo maelekezo yangu kwenu ni kuhakikisha kila Halmashauri kunakua na vikundi viwili mvipambanie hadi vinyanyuke.

Anzisheni vikundi viwili kwa kuanzia kwenye Halmashauri zenu, watengenezeeni mpango wa biashara kulingana na eneo walilopo kama ni biashara ya Dagaa au zao la Chai muhimu ni kuwanyanyua kupitia vikundi, na mimi kuanzia Novemba ntakua napita kwenye Halmashauri kukagua vikundi na sehemu ambayo itakua bado niwaambie ukweli tutakua wakali,"Amesema Ndejembi.

Naibu Waziri Ndejembi pia ameipongeza TASAF makao makuu kwa kuingia mkataba na Bodi ya Mikopo nchini ambayo itawasaidia wanafunzi wanaotokana na kaya maskini nchini kuhakikishiwa upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na Waratibu wa TASAF Mkoa wa Ruvuma ambapo amewataka kuanzisha vikundi viwili kwenye Halmashauri zao .
Waratibu wa TASAF Mkoa wa Ruvuma wakimsikiliza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi alipofika kuzungumza nao.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi akizungumza na Waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mkoa wa Ruvuma.

 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...