Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
BENKI ya Taifa ya Biashara Tanzania (NBC) rasmi imeingia kandarasi ya miaka mitatu na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kudhamini Ligi Kuu Soka Tanzania kwa kiasi cha Shilingi Bilioni 2.5 (kabla ya VAT) mkataba utakaonza msimu huu wa 2021-2022.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Theobald Sadi amesema kutokana na ubora wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Uongozi wa Benki hiyo umeona kuna umuhimu wa kudhamini Ligi hiyo ikiwa sambamba na lengo la kuinua kiwango cha Soka, kuleta sifa nchini.
Sadi amesema ubora wa Ligi hiyo umeendelea kuvutia Wachezaji mbalimbali wa Soka wa viwango vya juu zaidi Afrika. Hivyo kuleta chachu ya ushindani katika mchezo huo unafuatiliwa zaidi na watazamaji Milioni 40, kutambuliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwa ubora wake na kupewa nafasi adhimu kati ya Mataifa 12 ya Afrika kuwakilisha nchi zao katika Michuano inayosimamiwa na Shirikisho hilo la CAF.
“Uongozi wa NBC umefanya uamuzi kuingia mkataba wa miaka mitatu na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuwekeza Shilingi la Kitanzania Milioni 2.5 (kabla ya VAT) kuanzia msimu wa kwanza wa 2021-2022”, amesema Sadi.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amesema kipindi hiki Ligi Kuu ya Tanzania Bara imekuwa bora zaidi kutokana na udhamini huo wa Kampuni mbalimbali wakiwemo Azam Media, amesema uwekezaji huo umefanya Ligi hiyo kuwa bora zaidi na kuwa kwenye nafasi nzuri Afrika.
Karia amesema Ligi hiyo ya Tanzania katika kipindi cha miaka minne ilikosa hadhi kutokana na kukosa mvuto ikiwemo kukosekana kwa rasilimali fedha za kuendesha Ligi husika. Amesema kwa sasa baada ya uwekezaji huo imekuwa na hadhi na kuwa ubora na kutambulika Afrika kwa ubora huo hadi kufika nafasi ya nane na kupewa nafasi ya upekee pamoja na mataifa mengine 11 katika Michuano ya Vilabu Afrika.
“Nawapongeza NBC kutambua umuhimu wa Ligi yetu ya Tanzania na kuwa Wadhamini wakuu wa Ligi hii, wamekuwepo Azam Media wao wameingia mkataba mrefu na sisi kutoka na uwekezaji wao mkubwa katika vifaa. NBC wao tunawashukuru kwa kuongeza kitu katika miaka mitatu na wao kuwa Wadhamini wakuu wa Ligi yetu kuanzia msimu huu wa 2021-2022”, ameeleza Karia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...