Na Mwandishi wetu, Babati

MWENDESHA mashtaka wa Mahakama ya Mkoa wa Manyara, Mutalemwa Kishenyi ameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Manyara, katika kesi ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni tano.

Hakimu Mfawidhi Elimo Massawe ametoa uamuzi huo ambapo ameisoma hukumu hiyo kwa njia ya mtandao akiwa Singida kwa sababu ya kubanwa na majukumu ya kikazi. 

Hakimu Massawe amesema Mahakama hiyo imeakua  kumuachia  huru kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Hakimu huyo amesema Mahakama inamuachia huru kwa mujibu wa kifungu cha 235 mshtakiwa baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zinamkabili.

Awali amedai kuwa hati ya mashtaka ilionyesha kuwa mshtakiwa aliomba na kupokea rushwa shilingi milioni tano kutoka kwa Gasper Mlay  kinyume na kifungu  15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa ya mwaka 2007.

Massawe amesema Mlay alikuwa anampatia rushwa hiyo ili aweze kumsaidia kumshawishi kuondoa baadhi ya makosa kwenye maelezo ya wafanyakazi wake yaliyokuwa yameandikwa kituo cha polisi Babati.

Amesema baada ya kusikiliza pande zote mbili hakuna ushahidi wa mawasiliano uliothibitisha kuwa mshtakiwa alipokea fedha hiyo au kuthibitisha kuwa polisi walishirikiana naye ili aondoe maelezo ya watu wengine.

Hakimu huyo amesema kwenye hati ya mashtaka   ilionyesha Gasper Mlay ni mfanyakazi wa kiwanda cha Malt Super Brands Ltd wakati siyo kweli kama ilivyoelezwa kwenye hati hiyo.

Amesema mashahidi wa upande wa utetezi akiwemo Mkurugenzi wa kiwanda cha Malt Super Brands Ltd David Mulokozi alimkana Mlay kuwa hakuwa mfanyakazi wa kampuni hiyo.

Hakimu huyo amesema shauri hilo lilifikishwa mahakanani hapo Aprili 27 mwaka huu na kuanza kusikilizwa.

Hata hivyo, wakili wa utetezi Thadey Lister akizungumza baada ya uamuzi huo amesema shauri hilo la jinai  namba 24 la mwaka huu limeendeshwa mfululizo kwa wiki mbili likisimamiwa na Hakimu Mfawidhi Elimo Massawe kutoka mkoa wa Singida.

"Mahakama imemuachia huru mteja wangu baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi watano na vielelezo sita huku upande wa utetezi ukiwasilisha vielelezo tisa na mashahidi wawili," amesema Lister.

Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara, Martine Makani amesema mshtakiwa huyo Mutalemwa alikuwa anakabiliwa na kosa la kupokea rushwa.

"Mahakama imeamua kumtumia Hakimu Mfawidhi wa mkoa wa Singida ili kuepuka watu kulalamika kuwa mahakama haijatenda haki kwa kuwa mshtakiwa alikuwa akifanya kazi kwa ukaribu na idara hiyo," amesema Makani.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...