Na John Walter-Manyara.


Mkoa wa Manyara unatajwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa vitendo vya Ukatili hasa Ukeketaji, ambapo kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya Afya na Malaria Tanzania wa Mwaka 2015/2016, (Tanzania Demographic and Health Survey and Malaria Indicator Survey TDH-MIS 2015-2016) ni kwamba mikoa ya Mara, Arusha, Dodoma,Manyara na Singida ndio inayoongoza kwa ukeketaji wa wanawake nchini Tanzania.


Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mikoa hiyo inayoongoza kwa ukeketaji inaongozwa na Manyara wenye asilimia 58 ukifuatiwa na Dodoma(47), Arusha(41), Mara(32)na Singida yenye asilimia 31.
Hii ina maana kuwa kila wanawake 10 waliopo mkoani Manyara, sita wamekeketwa jambo linalorudisha nyuma mapambano ya kuzuia vifo vya akina mama na watoto.


Hata hivyo serikali katika kuibadilisha jamii kuachana na mila potovu na zilizopitwa na wakati inashirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa jamii ambapo shirika lisilo la kiserikali la FARAJA YOUNG WOMEN’S DEVELOPMENT ORGANIZATION (FAYOWODO) kikiongozwa na mkurugezi wake Martina Siara, limeonesha matumaini makubwa katika mradi wao wa kupinga ukeketaji unaotekelezwa wilayani Longido mkoa wa Arusha na Maeneo ya wilayani Babati mkoani Manyara.


Kiongozi wa mradi wa kupinga Ukeketaji unaotekelezwa na (FAYOWODO) Sambeke Melubo Kiruswa amesema kuwa tangu kuanza mradi huo wa kutoa semina kwa wananchi kwenye eneo la mradi katika wilaya ya Babati kwenye kata za Mamire, Mwada na Nkaiti mabadiliko ya kupunguza ukeketaji yameanza kuonekana ambapo baadhi ya mangariba wamekubali kuacha ukatili huo na kuungana na shirika hilo kutoa elimu kwa mangariba wengine ili waache kukeketa na hatimaye kuondosha kabisa suala hilo ambalo pia humwaathiri mtoto wa kike kisaikolojia.


Kwa upande wake ngariba aliyeacha shughuli ya ukeketaji na kuungana na shirika hilo Magreth Baso amesema kuwa walikua wanafanya shughuli hiyo kujitafutia pesa kwa kuwa hawakujua athari zake lakini baada ya kupata elimu hiyo yeye na wenzake wameamua kuacha na kutoa elimu kwa jamii.
Anasema mtoto mmoja alikuwa akimkeketa kwa shilingi elfu kumi na tano na hufanya hivyo katika kipindi cha kiangazi.

 Anasema sababu nyingine ya kukeketa mabinti kwa baadhi ya jamii kama Wairaq walikuwa wakiamini kwamba mtoto wa kike akiachwa nyumbani mwenyewe atakutana na wanaume hivyo alikuwa anakeketwa ili akose hisia katika tendo la ndoa.


Ameongeza "Mwanamke haolewi kama hajakeketwa na endapo mwanaume akioa mwanamke asiyekeketwa lazima mwanaume atapata laana na kutengwa na jamii".


Aidha mwenyekiti wa kijiji cha Mwinkatsi kilichopo kata ya Mamire wilayani Babati mkoani humo Peter Edward ameeleza kuwa kwa elimu waliyoipata kutoka katika shirika hilo, kwenye vikao vyake vya kijiji miongoni mwa ajenda ni pamoja na Elimu ya kupinga vitendo vya kikatili.


Mbunge wa Babati Vijijini Daniel Sillo amelaani na kukemea vikali vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea katika jamii na amewataka wananchi katika jimbo lake kushirikiana katika kukabiliana na vitendo hivyo nchini.


Katika hatua nyingine amelipongeza shirika la Faraja kwa kuchukua hatua hiyo madhubuti ya kukabiliana na ukatili katika jamii.Aidha Sillo amekifungua kikundi cha Wajasirimali wanawake kijiji cha Mwinkatsi kinachojulikana kama Haidadonga.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...