WASIRI wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako, amesema Wizara itahakikisha Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyoko Zanzibar inajengewa Maabara  za muda na kuwekewa vifaa baada ya moto kuteketeza maabara zote na vifaa siku ya Jumamosi Oktoba 2, 2021 ili kuwezesha wanafunzi kuendelea na masomo watakapofungua chuo.  

Akizungumza Zanzibar Oktoba 4, 2021 baada ya kukagua uharibifu uliotokea kwenye jengo la maabara la Taasisi hiyo lililoko eneo la Mizingani Bandarini, Waziri Ndalichako amesema pamoja na kujenga maabara za muda Wizara ina mpango wa kujenga maabara za kudumu na kwamba tayari Serikali kupitia Wizara ilishatoa Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara mpya, hivyo ameagiza sehemu ya fedha hizo zitumike kununua vifaa muhimu vya maabara  zitakazotumika  kwa muda.

"Sisi kama Wizara tunaendelea kutekeleza kwa vitendo maono ya  Rais ya kuhakikisha elimu yetu inatoa vijana wenye ujuzi katika eneo hili la sayansi za bahari na ndio maana wiki iliyopita tumetoa kwa Taasisi hii Shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukamilisha maabara mpya, hivyo pateni kibali cha kutumia sehemu ya fedha hizo kununua vifaa," Amesema Waziri Ndalichako.

Aidha, Prof Ndalichako amemuagiza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye   kuhakikisha Chuo kinafunguliwa Oktoba 25, 2022 kama ilivyopangwa ili  kutoathiri mzunguko wa Mwaka wa Masomo na kuwataka wanafunzi wa Chuo hicho kutokuwa na hofu .

Ndalichako ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jeshi la Polisi, Idara ya Zimamoto kikosi cha Bandarini na  Kamisheni ya Maafa iliyoko chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar pamoja na Raia wema kwa kazi kubwa ya kudhibiti na kuzima moto huo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar, Simai Mohamed Said amemshukuru Prof. Ndalichako kwa kufika katika eneo hilo na kuahidi  kushirikiana na chuo hicho kuhakikisha shughuli za Masomo zinaendelea kutokana na umuhimu wa Taasisi hiyo kwa uchumi wa nchi.

"Sote tunatambua umuhimu wa Taasisi hii ambayo ni chachu na kitovu cha kuimarisha uchumi wa Buluu na maabara hizi zilikuwa tegemeo si kwa Tanzania tu bali hata nchi za jirani hivyo tutashirikiana kuhakikisha zinarejea katika kipindi kifupi," amesema Simai.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam  amesema moto huo ulizuka Jumamosi mchana  katika jengo la  maabara eneo la Mizingani Bandarini na kuteketeza maabara zote 3  pamoja na vifaa, vyumba vya madarasa 3, ofisi 2  na chumba cha "Server".

Amesema Taasisi mbalimbali na jeshi la polisi zinaendelea na uchunguzi ili kubaini hasara halisi na kuongeza kuwa Chuo tayari kimeandaa mpango wa kuwezesha masomo kuendelea mara kipindi cha masomo kwa mwaka 2021/2022 kitakapoanza Oktoba 2021. Amesema mpango huo ni Pamoja na kujenga maabara za muda katika eneo la Buyu yalipo makao makuu ya Taasisi hiyo.

Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salam iliyopo Zanzibar ina wanafunzi zaidi ya 100 wa Shahada ya Awali, Umahiri na Uzamivu kutoka Tanzania na nje ya Tanzania.

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia uharibifu wa miundo mbinu ya maabara za Taasisi ya Sayansi za Bahari  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zilizoteketea kwa moto  Oktoba 2 , 2021 katika eneo la Mizingani Bandarini Zanzibar.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa William William Anangisye akimuonesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako vifaa mbalimbali vya maabara za Taasisi ya Sayansi za Bahari vilivyoteketea kwa Moto.
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  Simai  Mohamed Said pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prof James Mdoe wakikagua Maabara za Taasisi ya Sayansi za Bahari  ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zilizoteketea kwa moto Jana   Oktoba 4 , 2021 katika eneo la Mizingani Bandarini Zanzibar.
 

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe,  Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar  es Salaam na viongozi Waandamizi wa chuo hicho wakikagua eneo zitakapojengwa maabara za muda za Taasisi ya Sayansi za Bahari katika kampasi ya Buyu


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...