Na Mwandishi Wetu-Michuzi Blog

TAMASHA la Kimataifa la Utamaduni Bagamoyo ambalo limefanyika kwa siku tatu limefungwa huku Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akitoa pongezi wa Wizara Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kutumia tamasha hilo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Bagamayo hasa historia ya utumwa.

Rais huyo mstaafu kabla ya kufunga tamasha hilo lililofanyika Viwanja vya Chuo cha  Taifa cha Sanaa na Utamaduni (TaASUBa) ameshuhudia burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali ndani na nje ya Tanzania na katika siku zote tatu maelfu ya wananchi wamejikoteza kwa wingi.

Akizungumza wakati akifunga tamasha hilo pamoja na mambo mbalimbali, Kikwete amepongeza Wizara hiyo kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya kufanikisha tamasha hilo na kubwa zaidi kuutangaza utali wa Bagamoyo.

Pia amesema amefurahi kuona wasanii wanatengenezewa mazingira bora zaidi ya kuhakiki na kudhibiti haki za kazi zao na kuhakikisha wanalipwa inavyostahiri.

Ameongeza  matumaini yake taasisi zote zinazosimamia sekta ya sanaa watafanya kazi kubwa ya kulinda kazi za wasanii ili sekta hiyo iweze kukua na kufika mbali kama matarajio yao.

Dkt.Kikwete amesema sanaa siku hizi inalipa kuliko zamani,imekuwa ajira ya uhakika na wasanii wanashindana na kuweza kuhakikisha sanaa na hata michezo kukua.

"Sanaa ni ajira, imeajiri watu wengi, zamani tulizoea kuona kuna Mbaraka Mwishehe,Dar Jazz,Sikinde,Kilwa Jazz lakini sasa hivi hata hauwezi kuhesabu idadi yake na inalipa," amesema Kikwete.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa  kuwapa moyo Wizara kuendeleza Tamasha hilo lenye  historia katika  Taifa la Tanzania.

“Kwa dhati kabisa nitumie fursa hii adhimu kumshukuru mama yetu, Mhe. Rais kwa kuona changamoto ya ufinyu wa bajeti unaoikabili Wizara yetu, hivi karibuni ameelekeza Wizara yetu na Wizara ya Fedha kukaa pamoja ili kufanyia kazi changamoto hii” ameongeza  Gekul.

Amefafanua kuwa Tamasha hili ndiyo Tamasha kongwe zaidi nchini na limebeba historia ya Taasisi ya Chuo cha Sanaa Bagamoyo.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Abubakar Kunenge ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuthamini mchango wa Tamasha hili ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara kuboresha tamasha hilo ambalo amesisitiza kuwa lina faida kubwa siyo tu kwa wakazi wa Bagamoyo bali kwa taifa zima.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainab Abdallah amemshukuru Dkt.Kikwete kuweza kufika katika tukio hilo pamoja na baadhi ya viongozi kuona umuhimu wa tamasha hilo na kuweza kufika kushiriki na wananchi wa Bagamoyo.

Amemshukuru Katibu Mkuu wa UVCCM Bw.Kenani Kihongosi kwa kuweza kushiriki tukio hilo linalowagusa vijana wa nchi hii ambalo limekuwa la kihistoria kwa mafanikio makubwa.

"Asanteni wote mliofanikisha tamasha la 40 la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kuwa la mafanikio makubwa sana. Mwisho wa tamasha hili ni maandalizi ya tamasha lijalo". amesema Zainab.

PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-MMG



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...