Waziri wa Mambo ya Nje, Biashara na Vivutio vya Kiuchumi wa Ufaransa Franck Reister akipanda gari linalotumia mfumo wa umeme (E-Motion) linalomilikiwa na kampuni ya Mount Kilimanjaro Safari Club ambalo ni zao la teknolojia kutoka nchini Ufaransa, Waziri Reister ameahidi ushirikiano zaidi na Tanzania hasa katika teknolojia.





Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

WAZIRI Wa Mambo ya Nje, Biashara na Vivutio vya Kiuchumi wa Ufaransa Franck Reister ameahidi kuendeleza ushirikiano wenye tija na mafanikio kwa mataifa mawili ya Tanzania na Ufaransa hasa katika sekta mbalimbali za kijamii na uchumi kwa kutumiaa teknolojia rafiki inayotunza na kuhifadhi mazingira.

Ameyasema hayo jana katika ubalozi wa nchi hiyo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuzindua magari mawili ya watalii yanayotumia umeme (E-Motion,) kutoka kampuni ya utalii ya Mount Kilimanjaro Safari Club na kuwataka watanzania kuona na kutumia fursa hiyo ya teknolojia ya kutumia magari yanayotumia umeme iliyo salama katika utunzaji wa mazingira.

Waziri Reister amesema kuwa ni fahari kubwa kutumia magari hayo yanayotumia mfumo wa umeme ambayo yametengenezwa na kampuni ya Ufaransa kwa ushirikiano wa karibu na chuo cha ufundi Arusha Tanzania.

''Hili ni gari la sasa na baadaye kwa kuwa linatumia umeme na halina athari kwa mazingira yetu, hakuna uzalishaji wowote wa gesi ya ukaa na kelele zitakazopelekea uharibifu wa mazingira kwa namna yoyote ile.'' Amesema.

Aidha amesema kuwa magari hayo yanayotumika kwa kiasi kikubwa katika sekta ya utalii na hifadhi mbalimbali pia yanaweza kutumika katika usafiri wa umma ili kukwepa uharibifu wa mazingira na kwa sasa Serikali kutoka nchi hizo mbili zipo katika mazungumzo yanayohusisha kampuni za nchi hizo katika suala la kushirikishana teknolojia na kudumisha uhusiano uliopo.

''Uhusiano wa Ufaransa na Tanzania ni madhubuti na tunafurahi sana kushirikiana na kampuni za Tanzania katika masuala ya teknolojia, tunaamini kujenga maendeleo kwa wananchi kwa kutumia teknolojia rafiki ni mafanikio makubwa ya kujenga jamii bora ya sasa na baadaye.'' Amesema Waziri Reister.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya Mount Kilimanjaro Safari Club George Olemen'garai amesema kuwa kupitia teknolojia hiyo kutoka nchini Ufaransa kwa miaka tisa sasa wamekuwa wakitumia magari hayo yanayotumia umeme kusafirisha watalii katika eneo la Gurumeti na hifadhi ya taifa ya Serengeti.

''Wanyama hawapendi kelele na magari haya ni njia sahihi kwa kuzuiaa kelele kwa wanyama pamoja na kutunza mazingira....na betri yake inakwenda umbali wa kilomita 130 na zaidi hii imetusaidia kwenda na kasi ya teknolojia kidunia hasa katika suala zima la utunzaji wa mazingira kwa kuepusha changamoto za kelele, uzalishaji wa hewa ya ukaa pamoja na changamoto ya mafuta pindi yanapopanda bei na matumizi ya gari hii huokoa gharama kwa kiasi kikubwa.'' Ameeleza.

Waziri Franck Reister alikuja nchini kwa ziara ya siku moja ambapo alizundua safari za ndege kutoka Paris, Ufaransa hadi Zanzibar, alikutana na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, kuzungumza na wafanyabiashara, wafanyakazi na raia wa Ufaransa waishio nchini pamoja na kufanya vikao na mawaziri mbalimbali na kujadili masuala mbalimbali ya kuendeleza ushirikiano.




Waziri wa Mambo ya Nje, Biashara na Vivutio vya Kiuchumi wa Ufaransa Franck Reister akizungumza na jumuiya ya wafanyabiashara wa Ufaransa nchini Tanzania katika makazi ya Balozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje, Biashara na Vivutio vya Kiuchumi wa Ufaransa Franck Reister akiwa katika picha ya pamoja na jumuiya ya wafanyabiashara wa ufaransa nchini Tanzania mara baada ya mazungumzo maalumu yaliyokutanisha mataifa mawili ya Ufaransa na Tanzania.


Waziri wa Mambo ya Nje, Biashara na Vivutio vya Kiuchumi wa Ufaransa Franck Reister akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili katika Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania na kueleza kuwa uhusiano uliopo baina ya mataifa hayo mawili ni madhubuti kwa kizazi cha sasa na baadaye.


Waziri wa Mambo ya Nje, Biashara na Vivutio vya Kiuchumi wa Ufaransa Franck Reister akizungumza na wageni mbalimbali waliokuja kumpokea katika viwanja vya Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania.























Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...