MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA (TRA), imewataka wafanyabiashara nchini kujiepusha na biashara za magendo wakati wanapofanya shughuli zao za kibiashara katika maeneo yao ili wao wenyewe pamoja jamii inayowazunguka wasiathirike na athari zitokanazo na biashara hiyo.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Afisa Forodha Mwandamizi wa TRA, Bw. Muhidini Mwalugoya wakati wa kampeni maalum ya utoaji elimu kuhusu athari za magendo katika mikoa ya ya Lindi na Mtwara.
Bwana Mwalugoya amesema kwamba kufanya biashara za magendo kunaweza kuleta athari nyingi katika jamii kiafya, kiuchumi na kiusalama wa nchi akafafanua kuwa, inapotokea wafanyabiashara wanaingiza bidhaa zao kupitia njia zisizo rasmi maarufu kama njia za panya, jamii ya eneo husika huathirika, kwa mfano uingizaji wa vyakula au bidhaa zisizo na viwango ama zilizopita muda wake wa matumizi kunaweza pelekea mlipuko wa magonjwa na kuathiri wananchi.
Aliongeza kuwa, athari nyingine zitokanazo na biashara ya magendo ni pamoja kiusalama wa nchi, baadhi ya watu wasio na lengo zuri ama waharifu wanaweza kuingiza nchini bidhaa ambazo ni hatari kwa usalama wa nchi, mfano kuingiza silaha au risasi ambazo baadaye zinaweza kusambaa katika jamii na kuleta machafuko.
“Watanzania wenzangu, athari za kufanya biashara za magendo ni nyingi hivyo lazima tuhakikishe kuwa tunaelimishana ili wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla waachane na kufanya biashara za namna hii, kwa mfano tukiendekeza kupitisha bidhaa kutoka nje ya kwa njia zisizo rasmi tunaweza kuathiri uchumi wa nchi yetu pia, kwasababu zitakua hazilipi kodi na matokeo yake tunakosa mapato stahiki ya kutuletea maendeleo nchini, hivyo niwaombe sasa tuachane na hizi biashara”, alisema Mwalugoya.
Aidha, amewataka wafanyabiashara na wananchi nchini kuhakikisha kuwa wanatumia njia zilizo rasmi katika kupitisha bidhaa zao ili TRA iweze kukusanya mapato na pindi wapatapo changamoto yoyote wasisite kuwasiliana na Maofisa wa TRA katika maeneo husika ikiwemo kutoa taarifa kwa vyombo vya Ulinzi na usalama mara waonapo baadhi ya watu au kikundi cha watu wanafanya biashara za magendo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kilwa Kivinje Wilayani Kilwa, Bw. Mohammed Msumeno alisema kwamba, anaishukuru TRA kwa kutoa elimu hiyo kwa jamii ya eneo lake na kuahidi kuiepeleka elimu hiyo kwa wengine na ametoa wito kwa wakazi na wafanyabiashara wa Kilwa Kivinje kuachana na biashara za magendo na kukemea vikali wale wanaofanya biashara hizo kwa kuwatolea taarifa pindi wanapobainika katika vyombo husika.
Mmoja wa Wafanyabiashara ambaye pia ni mvuvi wa eneo la Kilwa Kivinje, Bw. Nurdin Likwata alitoa maoni yake kuhusu elimu iiyotolewa na TRA kuhusu biashara magendo ambapo alisema kwamba, elimu hiyo wameipokea na wataizingatia kwasababu ina manufaa kwao na kwa vizazi vyao ambapo ameahidi kuwa mstari wa mbele kukemea wale wote watakaobainika kuendesha biashara ya namna hiyo.
“Kiukweli hii elimu tuliyopewa na hawa watu wa TRA tulikua wala hatuifahamu, tumeipokea kwa mikono miwili na mimi binafsi naahidi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba nakemea vikali biashara ya magendo, kwanza ina madhara makubwa sana kwetu sisi na hata kwa watoto wetu lakini pia tunaiomba TRA iendelee kutupatia elimu hii mara kwa mara”, alisema Likwata.
Elimu kuhusu biashara ya magendo nchini ni endelevu na ni moja ya vipaumbele vya TRA iliyojiwekea katika Idara ya Forodha katika kuhakikisha kwamba, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanaelimishwa ipasavyo kuhusu madhara yatokanayo na biashara ya magendo na hatua mbalimbali za kuchukua pindi waonapo watu wanajihusisha na biashara hiyo ikiwemo kutoa taarifa TRA pamoja na kwenye vyombo vya Ulinzi na Usalama ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Baadhi ya Wavuvi wa pwani ya Kilwa Kivinje wakifuatilia elimu kuhusu athari za magendo iliyokuwa ikitolewa na Afisa wa TRA (hayupo pichani) hivi karibuni wakati wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu atahri za magendo katika mikoa ya kusini ya Lindi na Mtwara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...