Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
TUZO za msimu wa Mashindano (2020-2021) za Shirikisho la Soka nchini (TFF) zimetolewa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam huku ikishuhudiwa Wachezaji wa timu za Wanaume na Wanawake nchini wakiondoka na Tuzo hizo katika vipengele tofauti.

Tuzo hizo zilizohudhuriwa na Mgeni rasmi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ambaye amepongeza Tuzo hizo kutambua vipaji vya Wachezaji, Makocha na Wadau wengine wanaohusika na mpira wa miguu. Tuzo hizo pia zilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Soka la Tanzania na wadau wengine wa michezo hususani mpira wa miguu.

Katika utaoji wa Tuzo hizo, Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara msimu uliopita ni Nahodha wa Simba SC, John Raphael Bocco ambaye amewabwaga Kiungo wa Yanga SC, Mukoko Tonombe na Clatous Chama wa Simba SC ambaye kwa sasa anacheza RB Berkane ya Morocco. Pia John Bocco ameibuka kuwa Mfungaji Bora wa Ligi hiyo.

Mchezaji Bora wa msimu uliopita kwenye Ligi Kuu ya Wanawake (Serengeti Lite Women Premier League) Kiungo wa Yanga Princess, Amina Bilali aliibuka kidedea katika kipengele hicho baada ya kuwabwaga Mshambuliaji Opah Clement wa Simba Queens na Aisha Masaka wa Yanga Princess.

Golikipa Bora wa msimu huo, Kipa wa Simba SC, Aishi Salum Manula ameondoka na Tuzo zote mbili katika Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup (ASFC) wakati kwenye kipengele cha tuzo (VPL) amewashinda Makipa, Haroun Mandanda wa Mbeya City FC na Jeremiah Kisubi wa Tanzania Prisons ambaye kwa sasa amesajiliwa Simba SC. Kwa upande wa Soka la Wanawake, Golikipa Janeth Shija wa Simba Queens ameibuka mshindi wa Tuzo hiyo.

Kiungo wa Yanga SC, Feisal Salum (Feitoto) katika kipengele cha Mchezaji Bora wa Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ameibuka na Tuzo hiyo akiwakilisha Wachezaji wa Yanga SC katika Tuzo ya Mchezaji mmoja mmoja katika vipengele vyote huku Beki wa kulia wa timu hiyo, Kibwana Shomari akiibuka na Tuzo ya mchezo wa kiungwana (Fair Play) aliyoipata katika mchezo wao dhidi ya Ihefu FC katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Beki Bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Beki wa pembeni wa Simba SC, Mohammed Hussein (Zimbwe Jr) ametwaa Tuzo hiyo baada ya kuwashinda Dickson Job SC na Kibwana Shomari wote wa Yanga SC. Tuzo ya Kiungo Bora wa msimu huo, Clatous Chama ameibuka kidedea baada ya kuwabwaga Mukoko Tonombe na Feisal Salum (Feitoto) wote wa Yanga SC.

Kocha Bora wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba SC, Didier Gomes Da Rosa ameondoka na tuzo hiyo baada ya kuwashinda George Lwandamina wa Azam FC na Fransic Baraza wa Biashara United ambaye sasa yupo Kagera Sugar. Soka la Wanawake Kocha Bora ni Edna Lema (Mourinho) wa Ya ya Princess yeye amewashinda, Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan Mgosi na Ally Mohammed wa JKT Queens.

Katika Tuzo ya Mwamuzi Bora wa msimu ilishuhudiwa pia, Mwamuzi Ramadhan Kayoko akitetea tena tuzo hiyo baada ya kutwaa mwaka jana sambamba na Mwamuzi Msaidizi, Frank Komba akitetea tena Tuzo ya Mwamuzi Msaidizi. Wakati huo huo Coastal Union FC ya Tanga ikitoka na tuzo ya timu yenye nidhamu katika msimu huo sambamba na Ruvuma Queens kwenye Soka la Wanawake.

Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi kwa Soka la Wanaume imeenda kwa Kiungo Mshambuliaji wa Coastal Union FC, Abdul Suleiman Sopu na Tuzo hiyo kwa upande wa Soka la Wanawake imeenda kwa Mchezaji wa Alliance Queens, Asha Juma.

Mfungaji Bora wa Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) Mshambuliaji wa Namungo FC, Reliant Lusajo ameibuka mshindi sambamb na Mfungaji Bora wa Soka la Wanawake katika Ligi yao ni Mshambuliaji wa Yanga Princess, Aisha Masaka. Wakati Goli bora la TPL akipewa Mchezaji wa Tanzania Prisons, Lambert Sabiyanka.

Nichalous Reynolds (BONGO ZOZO) ameibuka na Tuzo ya Mhamasishaji Bora baada ya kuwabwaga Msemaji Haji Manara wa Simba SC sasa hivi Yanga SC na Msemaji Masau Bwire wa Ruvu Shooting FC wakati Tuzo ya Heshima kwa Soka la Wanawake akipewa Maneno Tamba na Tuzo ya Heshima Soka la Wanaume akitunukuwa Rais wa Heshima wa TFF, Leodgar Tenga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...