*Mwaka wa kwanza waliopangiwa mkopo sasa wafikia 45,095
*Lengo ni wanafunzi wapya 70,000 kwa mwaka 2021/2022
*Fedha zaanza kutumwa vyuoni
*Orodha ya Tatu wiki ijayo

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya pili yenye wanafunzi 7,364 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 19.4 bilioni kwa mwaka wa masomo 2021/2022 unaotarajiwa kuanzia wiki ijayo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Ijumaa Oktoba (22, 2021) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru ilisema orodha hiyo iliyotolewa leo inafanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo hadi sasa kufikia 45,095 yenye kiasi cha TZS 119.3 Bilioni.

Badru ameongeza kuwa HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanaopangiwa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” amesema Badru.

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Tatu, Badru amesema imepangwa kutolewa Jumatatu, Oktoba 25, 2021 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao ya SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Orodha hii ya pili inajumuisha wanafunzi wenye sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wamekamilisha taratibu za udahili wa chuo kimoja … tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya tatu katika siku tatu zijazo, yaani Jumatatu Oktoba 25, 2021,” amesema Badru.

Wakati huohuo, Badru amesema HESLB imeshapokea fedha kwa ajili ya malipo kwa wanafunzi waliopangiwa mikopo awamu ya pili taratibu za malipo zimekamilika na fedha za wanafunzi zinatarajia kufika vyuoni kuanzia leo Ijumaa, Oktoba 22, 2021.

Kwa mujibu wa Badru, Serikali imetenga TZS 570 bilioni kwa ajili ya mikopo ya jumla ya wanafunzi 160,000. Kati yao, wanafunzi 70,000 watakuwa ni wanufaika wapya na wanafunzi zaidi ya 90,000 ni wale wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.

Aidha, Badru alisema HESLB inawasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...