*Kamishna wa Kinga na Tiba aelezea mikakati iliyowekwa na DCEA kukomesha dawa za kulevya.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
TANZANIA bila dawa za kulevya inawezekana!Ndio inawezekana kabisa iwapo kila mmoja wetu akiamua kushiriki kikamilifu kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Tunafahamu taasisi mbalimbali za umma na binafsi ambavyo zinashirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya (DCEA) nchini katika kuhakikisha biashara ya dawa hizo inakoma.Kwa sehemu kubwa ushirikiano huo umekuwa ukisaidia katika mapambano ya dawa za kulevya.
Hata hivyo katika kukomesha biashara ya dawa za kulevya, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya mbali ya kushirikiana na wadau wengine, yenyewe imekuwa na mikakati madhubuti wanayoitumia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, iwe usiku, iwe mchana, iwe asubuhi, iwe jioni.
Akifafanua kwa kina kuhusu mikakati hiyo Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Dk.Peter Mfisi anasema mkakati wa kwanza ni kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya.
Katika utekelezaji wa mkakati huo, Dk.Mfisi anasema Mamlaka imejikita katika ukusanyaji na uchambuzi taarifa za wanaojihusisha na dawa za kulevya kwa maana ya ukamataji wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya, kudhibiti uzalishaji wa dawa za kulevya(kilimo na uzalishaji) kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa zenye asili ya kulevya pamoja na kuandaa na kusimamia miongozo ya utekelezaji wa dawa za kulevya.
Mkakati wa pili wa Mamlaka hiyo ni kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya ambapo mkakati huo unalenga katika utoaji wa elimu kwa jamii ili kuipusha isiingie katika matumizi na biashara ya dawa za kulevya."Mkakati huu unatekelezwa kwa kutoa elimu kuhusu tatizo la daw za kulevya katika jamii, kuandaa miongozo ya uelimishaji na kuwaandaa walimu wa walimu."
Wakati mkakati wa tatu, Dk.Mfisi anasema ni Kupunguza madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.Mkakati huo umejikita katika utoaji wa tiba na ushauri kwa waraibu wa dawa za kulevya pamoja na jamii inayowazunguka, lengo ni uhakikisha waraibu wa dawa hizo wanapata tiba.
Hivyo kupunguza madhara ya kiafya,kijamii na kiuchumi.Katika kutekeleza mkakati huo miongozo ya matibabu huandaliwa , uratibu wa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya pamoja na kufanya usimamizi shirikishi katika vituo vinavyotoa huduma za tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya.
Dk.Mfisi amesema mkakati wa nne ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa na kwamba mkakati huo unalenga kuimarisha ushirikiano kwakuwa tatizo la dawa za kulevya hasa biashara ya dawa za kulevya ni suala mambuka na biashara inayofanyika bila mipaka.
"Maeneo ya msingi ya mkakati huu ni kutekeleza mikataba na miongozo ya kimataifa katika udhibiti wa dawa za kulevya, kushiriki mikutano ya kimataifa kuhusu udhibiti wa dawa za kulevya na kushirikisha wadau ndani na nje ya nchi katika mapambano ya dawa hizo,"amesema Dk.Mfisi wakati akielezea hatua kwa hatua jinsi mikakati ya Mamlaka hiyo inavyofanya kazi.
Kuhusu juhudi za Mamlaka hiyo katika udhibiti upatikanaji wa dawa za kulevya, Dk.Mfisi anasema Tanzania imeendelea kudhibiti na kupambana na tatizo la dawa za kulevya za mashambani kama vile bangi na mirungi pamoja na zinazozalishwa viwandani zikiwemo Cocaine na Heroin.
"Taarifa ya hali ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2020 inaonesha kuanzia Januari hadi Desemba 2020 jumla ya kesi 7,361 za dawa za kulevya ziliripotiwa nchini na kati ya hizo kesi 428 zilihusu dawa za kulevya za viwandani na kesi 6933 zilihusu dawa za mashambani.Watuhumiwa 8757 walikamatwa na dawa za kulevya za mashambani,"amefafanua Dk.Mfisi.
Akizungumzia matumizi ya dawa za kulevya, Dk.Mfisi anasema dawa za kulevya zinazotumika nchini Tanzania ni bangi, heroin, mirungi,cocaine, dawa tiba zenya asili ya kulevya pamoja na viyeyushi kama petroli na gundi.Hata hivyo bangi imekuwa na idadi kubwa ya watumiaji ingawa bado kuna changamoto ya upatikanaji wa takwimu halisi ya watumiaji.
"Dawa inayofuata kwa matumizi ni heroin ambapo mwaka 2014 majumuisho ya tafiti mbalimbali yalikadiria kuwa kati ya watu 250,000 hadi 500,000 walikuwa wanatumia dawa hiyo na kati yao 30,000 wakitumia kwa njia ya kujidunga.Mirungi ni dawa ya tatu na cocaine ni ya nne kwa watumiaji,"amesema.
Akielezea sababu zinazochangia matumizi ya dawa za kulevya, Dk.Mfisi anasema Tanzania kama ilivyo katika maeneo mengine duniani matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuleta changamoto katika jamii pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na changamoto hizo.
Ametaja baadhi ya sababu ni kukosekana kwa elimu ya kujitambua miongoni mwa vijana, hali ambayo husababisha kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwasababu ya kukosa uwezo wa kutambua changamoto zao na njia za kutatua changamoto hizo.
Sababu nyingine ni kutokuwa na ufagamu mzuri kuhusu madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya kiafya, kijamii na kiuchumi.Asilimia kubwa ya watu wanajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa lengo la kupata starehe , kujaribu kutafuta furaha, kuwa karibu na marafiki au kupunguza makali ya maisha bila kufahamu madhara wanayoweza kuyapata.
Dk.Mfisi amesema sababu nyingine ni utandawazi na matumizi ya mitandao ya kijamii imekuwa kichocheo cha jamii na hasa vijana kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.Pia imani potofu, mila na desturi za baadhi ya jamii zimekuwa zikichangia matumizi ya dawa za kulevya.
"Migogoro na utengano wa familia imekuwa ikisababisha kukosekana kwa malezi bora kwa watoto na vijana hali inayosababisha kukosekana kwa uangalizi wa karibu na hivyo baadhi yao kujiunga na makundi yanayotumia dawa za kulevya.Wazazi wenye uraibu wa dawa za kulevya wana uwezekano mkubwa wa kupata mtoto mwenye tatizo hilo(urithi),"amesema Dk.Mfisi.
Kamishna wa Kinga na Tiba Dk.Peter Mfisi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...