Na Karama Kenyunko Michuzi TV 

HUKUMU ya kesi dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Evance Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange marufu kama Kaburu imeahirishwa hadi Oktoba 21, 2021 baada ya hakimu anayesimamia kesi hiyo kutaka apewe muda wa kupitia vizuri hoja za majumuisho ili kutoa hukumu kwa usahihi.

Hukumu hiyo iliyokuwa isomwe mapema leo Oktoba 6, imehirishwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Ipyana Mwakatobe huku washtakiwa wakisimama bila mawakili wao kuwepo.

Mapem wakili wa Serikali Ipyana Mwakatobe amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilipelekwa kwa ajili ya kusomwa hukumu na upande wa mashtaka walikuwa tayari kwa hukumu hiyo.

Hakimu Simba alisema kuwa kutokana na hoja za majumuisho kumfikia ndani ya kipindi kifupi huku yeye akiwa na majukumu ya kesi nyingine alihitaji muda wa kuzipitia kabla ya kutoa hukumu.

"Ukiangalia kwenye hili jalada utaona kuna hoja za majumuisho zimeletwa, kuna kesi zimenukuliwa humu na vifungu vya sheria, hivyo nahitaji muda wa kuzipitia kwa umakini ili nitoe hukumu kwa usahihi, hasa ukiangalia kuna hoja za majumuisho nyingine zimewasilishwa leo," alisema Hakimu simba.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na jumla ya mashahidi 10 na vielelezo mbalimbali huku washtakiwa wakijitetea wenyewe.

Awali Aveva na Kaburu walikuwa wakishtakiwa pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili Zachariah Hans Pope, ambaye amefariki mwezi uliopita

Katika kesi hiyo, Aveva na Nyange walikuwa wakikabiliwaa na mashtaka tisa ambapo Septemba 19, 2019 mahakama hiyo iliwaondolea mashtaka mawili ya utakatishaji fedha kwa kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuyathibitisha.

Hata hivyo, Mahakama hiyo iliawakuta na kesi ya kujibu katika mashtaka saba ambayo ni kughushi, kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa nyaraka za uongo, na kutoa maelezo ya uongo ambayo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha.

Katika shtaka la kwanza, Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.

Shtaka la pili Aveva na Nyange wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

Shtaka la tatu linalowakabili Aveva na Nyange inadaiwa kwa pamoja walighushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa Dola za 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

Katika shtaka la nne Aveva katika banki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa Dola za Kimarekani 300,000.

Shtaka la tano linawakabili Aveva, Kaburu na Hans Poppe ambao wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya Dola za Kimarekani 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli.

Katika shtaka la sita, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo kwa Levison Kasulwa kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Shtaka la mwisho Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...