Na John Walter- Manyara.
Wazee wa Kimila katika kata ya Ayalagaya wilayani Babati mkoani Manyara wamewapiga faini ya kulipa ng'ombe dume watatu kwa kosa la kuingia kijijini hapo na kuanza kufanya kazi kwenye chanzo kilichopo kijijini hapo bila kutoa taarifa kwao.
Wazee hao wametoa tamko hilo mbele ya mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro oktoba 11,2021 alipofanya ziara yenye lengo la kufanya upatanisho kati ya viongozi wa wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira mjini Babati (BAWASA) na wakazi wa vijiji vya Ayalagaya, Haysam na Gajal kwa madai ya mafundi wa BAWASA kuharibu chanzo cha maji katika mto Endalo na kusababisha maji kukosekana kwa siku saba.
Akitoa maelezo mbele ya mkuu wa mkoa Diwani wa Kata ya Ayalagaya Sabini John alimwabia mkuu wa mkoa kwamba, Mafundi hao waliingia kwenye chanzo kinachotumika na wakazi wa vijiji hivyo na kuanza kufanya shughuli za kutaka kusambaza maji katika vijiji vingine bila elimu kutolewa kwa wakazi wa vijiji husika.
Bw. John alieleza kuwa, mafundi hao bila taarifa walisababisha maji kuchafuka kwa kuchan’ganywa na saruji kitendo kilichowafanya vijana kuelekea sehemu ya chanzo hicho na kuwakuta mafundi hao ambao walichukuliwa hadi ofisi ya kijiji kwa kuchukuliwa maelezo ambayo hayakupokelewa hadi mkuu wa Wilaya Babati Lazaro Twange kuingilia kati.
“Mafundi waliingia msituni kwenye chanzo bila kusaini kwenye ofisi ya kijiji, vijana waliopandisha kwenye chanzo na kuwakuta walikuwa wastaarabu sana kwani hawakuwafanyia fujo yoyote zaidi ya kuwafikisha ofisini salama na hatimae kuwaruhusu waende hadi mwafaka upatikane” alisema.
Aidha mkuu wa mkoa alipokutana na wananchi wa vijiji hivyo jambo la kwanza aliwaruhusu watoe kero zao kwanza ndipo naye aweze kutoa majibu ya hoja zao bila kuathiri upande wowote na kuweza kupata muafaka wa yaliyotokea na kusababisha taharuki kwa wakazi hao.
Baada ya maelezo ya pande mbili kutolewa mbele ya mkuu wa mkoa huo ilionekana mafundi wa Bawasa walikuwa wakifanya shughuli zao bila kuwashirikisha viongozi wa kata husika ya Ayalagaya.
Akiongea kwa niaba ya wazee walioshiriki mkutano huo wa mkuu wa mkoa mzee Michael Tsaghara aliuambia mkutano kuwa, mafundi wameomba msamaha, hivyo wazee wamesema msamaha utakubalika endapo watalipa faini ya kulipa madume watatu wa ng’ombe watakaochinjwa na kuliwa hapo kwenye uwanja wa mikutano.
Mafundi hao wakiongozwa na Mhandisi Rashidi Cherehani wameridhia kulipa faini hiyo na tayari wako sokoni wakiwasaka madume hao watatu watakaowasilishwa uwanjani tayari kwa kitoweo cha wazee wa kata nzima na majirani zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...