Wito umetolewa
kwa wanachama wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kuwa
wasimamizi na wafuatiliaji wa mali Pamoja na uendeshaji wa shughuli za
vyama vyao vya Ushirika ili kuongeza tija na ukuaji ya Vyama vya
Ushirika nchini.
Hayo yamesemwa kupitia Hotuba ya Waziri wa
Kilimo Mhe. Prof. Aldolf Mkenda iliyosomwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife wakati wa kilele cha
maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na
Mikopo Duniani (ICUD) 14 Oktoba, 2021, yaliyofanyika mkoani Morogoro
Katika
hotuba hiyo Waziri amewataka wanachama kutimiza wajibu wao kwa
kushiriki kupata viongozi bora wa vyama, kutoa huduma zenye ubunifu na
uadilifu katika utendaji. Aidha, amewataka wanaushirika kuwa makini
katika uwekezaji bora wa rasilimali za vyama vyao vya ushirika. Hivyo,
Serikali itaendelea kuwaunga mkono.
“Serikali kwa kutambua
umuhimu wa Sekta ya Ushirika hasa Ushirika wa kifedha imekuwa ikichangia
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, niwahakikishie kuwa
tutasimamia ushirika kwa kuzingatia Sheria na kuhakikisha kuwa
hautetereki,” alisema Prof. Sife
Sambamba na hilo Mrajis wa Vyama
vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt.
Benson Ndiege amewataka wanachama wa vyama vya Ushirika kufuatilia
utendaji wa vyama vyao ili kuhakikisha usimamizi unaimarika katika vyama
na Hati safi za ukaguzi zinaongezeka
“Mtu wa kwanza wa
kuhakikisha chama kinapata hati safi ni mwanachama wa chama cha ushirika
kwa kufika kwenye mikutano inapoitishwa, kushiriki kwenye maamuzi yenye
maslahi kwa chama ni lazima tubadilike na kusimamia mali zetu nguvu ya
ushirika lazima ianzie kwa wanachama wenyewe,” alisema Mrajis
Aidha,
Mrajis amesema ni wakati sahihi sasa kwa vyama vya Ushirika wa mazao
kuwa na vyama vya Akiba na Mikopo ili kuongeza mzunguko wa fedha kwa
wakulima hasa kuwawezesha kumudu gharama mbalimbali za kilimo wakati wa
misimu ya mazao.
Dkt. Ndiege ameongeza kwa kutoa rai kwa vyama
ambavyo bado havijaomba Leseni za uendeshaji wa Vyama vya Ushirika wa
Akiba na Mikopo kwa mujibu wa Sheria Na.10 ya Huduma Ndogo za Fedha ya
mwaka 2018 kufanya hivyo ili kuendana na matakwa ya Sheria, Kanuni na
Taratibu zinazolenga kuongeza ufanisi wa vyama.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SCCULT) Dkt.
Gervas Machimu ameeleza lengo la maadhimisho hayo ni kuwaenzi na
kukumbuka mchango wa waasisi wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo,
wanaushirika kukaa pamoja kubadilisha uzoefu na kutathmini mchango wa
SACCOS katika maendeleo ya nchi.
Akieleza baadhi ya changamoto
zinazokabili Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo amesema bado vyama
hivyo vinakabiliwa na changamoto katika ukokotoaji wa gharama za malipo
ya kodi, ugumu wa kupata tafsiri za kisheria za Ushirika hasa katika
utatuzi wa migogoro wa kesi za ushirika ili kufikia muafaka na utatuzi
kufikiwa kwa haraka.
Mwenyekiti huyo ameshauri kuwa vyama vya
Ushirika wa Akiba na Mikopo kuendelea kushiriki katika michakato ya
mabadiliko ya Sheria Pamoja na mapitio mengine ya maboresho na
mabadiliko ya mifumo ya Ushirika hapa nchini.
Makamu
Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU) Prof. Alfred Sife akikabidhi
tuzo kwa Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Arusha Emmanuel Sanka kwa niaba ya
Chama Bora cha Ushirika chenye Leseni daraja A, Arusha Teachers saccos
wakati wa Kilele cha maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Ushirika wa
Akiba na Mikopo, Mkoani Morogoro.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe.
Dkt.Christine Ishengoma akitoa salamu za kamati wakati wa kilele cha
maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo (ICUD),
Mkoani Morogoro
Mrajis
wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika
Dkt. Benson Ndiege akielezea suala la Ushirika wakati wa Kilele cha
maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo, Mkoani
Morogoro
Home
HABARI
WAZIRI MKENDA AWATAKA WANACHAMA WA VYAMA VYA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO KUTIMIZA WAJIBU WAO KUPATA VIONGOZI BORA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...