SERIKALI Wilayani Ulanga, Morogoro imetaja fursa tisa zinazopatikana katika Wilaya hiyo ambapo imetoa wito kwa watanzania kuzichangamkia katika kuwekeza na kufanya biashara.
Mwito huo umetolewa leo na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ngollo Malenya wakati akizungumza na wandishi wa habari kuhusu uwepo wa Tamasha la kuhamasisha wawekezaji katika Wilaya ya Ulanga litakalofanyika Oktoba 22 na 23 katika Uwanja wa Mapinduzi uliopo Mjini Mahenge.
DC Malenya amesema lengo la tamasha hilo ni kutangaza fursa zilizopo wilayani humo pamoja na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuitangaza na kukuza pato la Taifa.
"Lengo la Tamasha hili la kuhamasisha uwekezaji katika Wilaya ya Ulanga linajulikana kama ULANGA IHEREPA, yaani AMAZING ULANGA, ULANGA KUNAPENDEZA, neno” Iherepa” lina maana inapendeza kwa lugha ya wenyeji wa Wilaya ya Ulanga WAPOGORO. Kauli mbiu ya Tamasha hili ni ‘‘TWENZETU ULANGA’’ Amesema DC Malenya
DC Malenya amesema pamoja na mambo mengine ya uwekezaji wanatarajia kuwa na michezo mbalimbali kama vile Riadha, kupanda milima (Hiking), Mbio za baiskeli (Mountain biking) pamoja na Ngoma za asili.
Aidha wageni kutoka ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kutembelea maeneo ya vivutio ikiwa ni pamoja na utalii wa mazingira ya asilii, utalii wa majengo ya kihistoria, utalii wa hifadhi za misitu pamoja na kufanya utalii wa kuvua samaki.
Amezitaja fursa zilizopo katika Wilaya hiyo kuwa ni fursa katika sekta ya Madini, sekta ya kilimo na ufugaji, uzalishaji wa asali, utalii, uvuvi, ngoma za asili na majengo ya kihistoria.
" Wilaya yetu ina fursa za uwekezaji katika tafiti za madini, uchimbaji wa madini, ubia na wamiliki wa leseni za maeneo ya madini ambao wana leseni lakini hawana mitaji, vifaa na teknolojia ya uchimbaji wa madini. Aina ya madini yanayopatikana Wilayani Ulanga ni pamoja na Madini ya Kinywe (Graphites), Rubi na Dhahabu.
Wilaya ya Ulanga ina eneo lenye ukubwa wa hekta 1,068,889.43 ambapo kati ya hekta hizo ni hekta 269,775.34 ambazo sawa na 23.95% zinafaa kwa shughuli za kilimo na hekta 11,714 zinatumika kwa kilimo cha umwagiliaji," Amesema DC Malenya
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...