
Wachezaji wa timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani (kushoto) wakivutana na wenzao wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake kwenye michuano ya Shirikisho la michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani. Tamisemi wamewavuta kwa 2-0.

Mchezaji Bakari Kibiki wa Ofisi ya Makamu wa Rais (kushoto) akichuana na Ambakisye Mwasunga wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) katika mchezo wa bao wa hatua ya makundi kwa wanaume kwenye michuano ya Shirikisho la michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Mwasunga ameshinda 2-0.


Timu ya wanawake ya Idara ya Mahakama (kushoto) wakivutana na Wizara ya Kilimo katika mchezo wa Nane bora wa michuano ya Shirikisho la Michezo ya Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri, ambapo Mahakama walishinda kwa mivuto 2-0.
********************************
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Timu za Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi zimeibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa wa mchezo wa karata kwa wanaume na wanawake kwenye michuano ya Shirikisho la Michezo kwa Idara na Wizara za Serikali (SHIMIWI) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Mchezaji Tuombe Alphonce wa Wizara ya Maji alimshinda Stephano Mjema wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika mchezo wa fainali kwa pointi 2-1; huku Sakina Chamshama wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi amemfunga Stella Telengelwa wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa pointi 2-0.
Nafasi ya tatu kwa wanaume imechukuliwa na Abdu Chalamande wa RAS Shinyanga aliyemshinda Paschal Banzi wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa alama 2-0; wakati kwa wanawake aliyeshika nafasi ya tatu ni Ambiliasia Minja wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) aliyemfunga Mayasa Mlula wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera.
Kwa upande wa mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake uliokuwa hatua ya Nane bora timu ya Idara ya Mahakama waliwavuta Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa 2-0; nayo Ofisi ya Waziri Mkuu Sera waliwavuta Hazina kwa 2-0; huku RAS Iringa waliwavuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) kwa 2-0 na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waliwashinda Wizara ya Mambo ya Ndani kwa 2-0.
Mechi hizo za nusu fainali zitafanyika kesho ambapo kwa wanaume timu zilizofuzu ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Idara ya Mahakama, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mh. Martin Shigela jana amesema hakuna sababu kwa mwaka 2022 timu zilizoshiriki mwaka huu kushindwa kushiriki na badala yake ziongezeke Zaidi ili kuleta ushindani mkubwa baina ya timu, ambapo pia watumishi wanaposhiriki wanaongeza ufanisi mahala pa kazi kutokana na kuwa na afya njema.
“Mtumishi wa Umma anapoingia kwenye mashindano anajengewa uwezo wa kufanya kazi kwa makini na bidii, hiyyo wanapokuja kucheza katika mashindano kunawaongezea vitu Fulani akilini na mwilini mwao,” amesema Mh. Shigela.
Wakati huo huo, mchezo wa kuendesha baiskeli itafanyika kesho kwa upande wa wanawake ni kilometa 24.5 zitakazoanzia Njiapanda ya Kilosa na kumalizikia eneo la Mafiga, huku kwa wanaume ni kilometa 35 zinazoanzia Kijiji cha Malecela na kumalizia eneo la Mafiga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...