Wakazi wa Kigamboni wanatarajia kupata huduma ya majisafi, salama na kutosheleza ifikapo mwezi Aprili mwaka 2022 kupitia Mradi wa Kisarawe II utakaosaidia kuondoa kero ya Maji katika Kata saba za wilaya ya Kigamboni kutokana na kuchimba visima na kujenga tenki la maji litakalokuwa linaweza kuhifadhi maji lita Milioni 15. Hii ni kutokana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam(DAWASA) kutenga fedha kwa ajili ya miradi hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mara ya kumaliza ziara hiyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemtaka Mkandarasi wa mradi huo Advent Construction Tanzania kubadili mfumo wa kazi kwa kufanya kazi usiku na mchana kwani vifaa vipo na pia wanaweza kuongeza nguvu kazi ili kumaliza mradi huo kwa wakati.
Amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa Wizara ya Maji kuhakikisha wananchi wa Dar es Salaam pamoja na Tanzania kwa ujumla wanapata majisafi na Salama ili kuweza kufikia lengo la kumtua mama ndoo kichwani inatimia.
Pia Aweso amewaomba viongozi wa dini kuendelea na maombi ili mvua ziweze kunyesha zenye manufaa na zisiwe na maafa ili kuweza kurudi kwenye hali ya kawaida ya kuzalisha maji zaidi ya lita milioni 520 maana kipindi hiki nicha mpito.
Pia Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Almasi Nyangasa amesema uongozi wa wilaya ya hiyo wanafuatilia kwa karibu na makini kwenye usimamizi wa mradi wa maji wa Kisarawe II wanashirikiana na DAWASA ili kuweza kuwapatia wananchi wa wilaya hiyo majisafi na salama.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi wa Maji Kisarawe II unahusisha uendelezaji wa visima kumi na mbili vya maji vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 57.
“Mradi huu unatekelezwa kwa sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni ujenzi wa kituo cha kusukuma maji, kituo cha kupokea Maji, ulazaji wa mabomba ya maji na ujenzi wa tanki kubwa la kuhifadhi maji la lita milioni kumi na tano linalojengwa Kigamboni na awamu ya pili ikihusisha kazi ya kufunga njia za umeme kwenye visima na kutoa maji kwenye visima na kupeleka kwenye kituo cha kusukuma maji amesema Luhemeja.
Luhemeja amesema Mradi huu ulianza kutekelezwa mwezi Disemba mwaka 2019 na unatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka 2022, huku ukigharimu kiasi cha bilioni 24 fedha za ndani za Mamlaka na kukamilika kwakwe kutanufaisha wakazi 250,000 wa maeneo ya Kibada, Mjimwema, Masonga, Kimbiji, Mpera na maeneo ya karibu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...