NA BALTAZAR MASHAKA, Ilemela
WANAFUNZI wa shule za sekondari Kilimani, Bujingwa na Buswelu,katika Manispaa ya Ilemela, wamemshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kutambua upungufu wa miundombinu ya madarasa na kutoa fedha za kujenga vyumba 15,000 nchini.
Walitoa shukrani na pongezi hizo jana mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandis.Robert Gabriel,wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba 11 madarasa kati 97 yanayojengwa wilayani Ilemela.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi hao Salvatory Emmanuel na Getrudeshose Kessy (Kilimani),Paulina Faustine na Aloys Martin (Bujingwa),Leokadia Aisha Bunu na Sekei Samike (Buswelu), walisema kuwa miundombinu hiyo itasaidia kuondoa msongamano na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Walisema kuwa Rais Samia kwa kuwasaidia kupata madarasa hayo ameonyesha mwanga na uzalendo kwa kujali elimu yao na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani ambapo walimwahidi kusoma kwa bidii na kufanya vizuri ili watimize ndoto zao.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa mchango wake wa fedha sh. milioni 40 za kujenga vyumba viwili vya madarasa, pia atusaidie kutatua na kufanyia kazi changamoto za Kilimani zilizoanishwa na Mkuu wa Shule,”alisema Emmanuel.
“Mama yetu Samia tunampongeza kwa kutambua changamoto za sekta ya elimu na kuamua kutoa fedha za kujenga madarasa,Kilimani ni sehemu ya kitovu cha taaluma hivyo rai yangu kwa serikali ya mkoa ione namna ya kushirikiana na wadau kujenga hosteli ili kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu bora,” alisema Kessy.
Martin wa Bujingwa sekondari alisema, "Rais Samia mama yetu ameonyesha moyo wa uzalendo wa kuboresha sekta ya elimu nchini, ni matumaini yetu kupitia kazi hii inayofanyika elimu itapanda kwa viwango vizuri,binafsi nitapata matokeo mazuri baada ya miaka saba ijayo nategemea kuwa kiongozi mkubwa katika Taifa hili."
Paulina yeye alisema kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia itatoa faida kwa wanafunzi kupata matokeo mazuri na kuahidi kuwa atakuwa kiongozi wa kutegemewa nchini baada ya kuhitimu masomo yake.
Pia Leokadia, alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia madarasa hayo yakikamilika,yatapunguza msongamano na yataongeza ari na morali ya wanafunzi kujifunza kwa bidii.
Aidha Samike, alisema serikali kwa kuwajengea miundombinu hiyo ya madarasa imetambua umuhimu wa elimu ya watoto masikini hivyo wanamwombea Rais maisha marefu huku Aisha Bunu akisema Rais Samia kwa kuonyesha kuwajali wanafunzi, watasoma kwa bidii na kufaulu kutokana na kuwezeshwa vyumba vya madarasa.
Awali akiwa Kilimani sekondari Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhandisi. Gabriel aliwaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kuonya wasichanganye mapenzi na masomo, wajiepushe na mimba za utotoni ili wafikie ndoto zao za maisha.
Alisema kila jambo duniani lina kanuni kadhaa za kuzingatia ili kupata mafanikio ni kufanya kazi kwa bidii na nidhamu,pia kwenye elimu ili kufanya vizuri katika masomo ni kusoma kwa bidii ukilala kwa saa 3 unafeli (fail).
“Hakuna njia ya mkato kwenye mafanikio, kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele,kuwa na maisha yenye nidhamu,hivyo ni muda wa kusoma si wakutafuta mchumba,masomo hayachanganywi na mapenzi,someni mtimize ndoto zenu.
Alieleza kuwa watu waliofanikiwa duniani wana nidhamu na kushauri wanafunzi hao kuwa bado ni watoto wadogo hivyo wasome kwa bidii wakitambua kuna nyakati mbalimbali za kupanda na kuvuna, jua na mvua,masika na kiangazi hivyo ni wakati wao wa kusoma.
"Ukilala saa 2 au saa tatu unafeli, ukifika nyumbani jioni fanya kazi za nyumbani na za shule, kama umepewa maswali kabla ya kulala fanya,Jumapili na Jumamosi msome na kabla ya mitihani ya Taifa fanyeni maswali ya mitihani ya miaka mitano nyuma au miaka 10 iliyopita hiyo itasaidia misuli yako ya uelewa iweze kuzoea,hakuna njia fupi kwenye mafanikio,"Mhandisi.Gabriel alisema.
Alishangaa mtoto wa kidato cha kwanza hadi cha nne kupata ujauzito aliyempa ujauzito yupo kidato cha pili, haeleweki leo ana mtoto nani anayemlea, shida anapeleka nyumbani na watoto watakuwepo tu hawaishi “muda wako wa kusoma tumia kusoma ili utimize ndoto yako huu ndio wosia wangu,”alisema.Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi. Robert Gabriel, akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilimani wakiwemo walimu wa shule hiyo jana baada ya kukagua ujenzi wa madarasa yanayojengwa kwa fedha za Uviko-19.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...