Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Barabara iliyokuwa inaleta changamoto ya usafiri kati ya Nzasa, Kata ya Kilungule na Buza kwa Mpalange, sasa inapatiwa ufumbuzi kwa maendeleo mazuri ya mradi wa ujenzi wa daraja litakalounganisha maeneo hayo bila changamoto yoyote kwa Watumiaji endapo litakamilika kwa wakati.
Imeelezwa kuwa gharama za Ujenzi wa Barabara, Daraja pamoja na Stendi ya Mabasi ya Buza unagharimu kiasi cha Pesa, Bilioni 19/-
Akizungumza na Michuzi Blog, Msimamizi wa Mradi huo katika eneo hilo, Mhandisi Rashid Said amesema kuwa mradi wa ujenzi wa daraja na njia hiyo ulianza Machi 2020 na unatarajiwa kukamilika Januari 2022 na kuwanufaisha watumiaji, tofauti na awali ambapo kulikuwa na changamoto kubwa hususani kipindi cha mvua.
Amesema awali kulikuwa na changamoto ya Maji mengi katika eneo hilo hali iliyopelekea Wakazi wa maeneo hayo wakiwemo wapita kwa miguu, Waendesha Magari sambamba na Madereva wa Bajaji, Bodaboda kushindwa kupita kutokana na kadhia hiyo ya kujaa kwa Maji.
“Tulichokifanya kwanza kutengeneza njia ya mchepuko (Diversion) kwa dharura ya kupitisha vifaa vyetu vya ujenzi, lakini imekuwa msaada mkubwa kwa Waenda kwa miguu na Waendesha Magari, kwa hiyo faida kubwa imeanza kuonekana hata kama mradi husika haujakamilika”, ameeleza Mhandisi Rashid.
“Tunaamini faida nyingi zitakuwepo baada ya kukamilika, ikiwemo ukuaji wa Uchumi baada ya kuwepo urahisi wa Barabara hiyo, Magari ya Abiria maarufu Daladala zitapita bila kadhia yoyote, Watu watafika kwa wakati kutokana na urahisi wa njia husika wanaenda Mbezi, Gongo la Mboto, wakitaka kutumia njia hii watatumia kwa urahisi kabisa”, ameeleza Mhandisi Rashid.
Kwa upande wa Watumiaji wa njia hiyo wameeleza unafuu unaopatikana sasa licha ya kuwepo kwa njia ya muda, tofauti na zamani hali ilikuwa tete, mmoja wa Watumiaji wa njia hiyo amesema Meshack Noel amesema mradi wa ujenzi wa njia hiyo utarahisi zaidi shughuli za usafirishaji katika maeneo hayo.
“Zamani Mvua zikinyesha Mlima huu maarufu kwa Mpalange, haupitiki kabisa maji yanajaa, njia inateleza, lakini kwa sasa tunashukuru kwa kweli Hali imebadilika na daraja, njia ikiisha kujengwa tutanufaika sana na usafiri rahisi”, amesema Meshack.
Naye Mkazi wa maeneo hayo, Saidi Maganga Ibrahim amesema kwa Hakika changamoto hiyo itakuwa imeisha kutokana na mradi wa ujenzi huo wa daraja na njia ya waenda kwa miguu, amesema zamani kulikuwa na changamoto kubwa usafiri kutokana na Mlima mrefu.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha maeneo ya Nzasa, Kilungule na Buza kwa Mpalange.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...