Upatikanaji
wa maji umekuwa mwiba kwa baadhi ya maeneo ya nchi, ambapo watu hupita
siku kadhaa bila kuyapata huku wengine wakikabiliwa na mgao.
Halikadhalika, Serikali imeshatoa hali ya tahadhari kwa watumiaji huku
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) ikiwaomba
watumiaji kuhifadhi maji kila yanapotoka. Hii ni kutokana na upungufu wa
kina cha maji katika maeneo ya Ruvu Juu na Mto Wami, changamoto
inayosababishwa na ukosefu wa mvua.
Hata hivyo, Waziri wa Maji,
Mhe. Jumaa Aweso amewahakikishia Watanzania kuwa ofisi yake inachukua
kila hatua ili kukabiliana na hali hiyo. Aidha, Waziri alisema wamekuwa
wakifanya mageuzi makubwa ya kitaasisi, kifedha na kiufundi ili kupata
huduma ya maji iliyo endelevu. Alisema, 'hadi sasa kuna wakala wa
usambazaji maji vijijini wapatao 2,115 unaojumuisha wahasibu 1,362 na
wataalam 1,611' katika maeneo ya vijijini’.
Wakati hayo yote
yakiendelea, kampuni pendwa ya bia, Serengeti Breweries Limited (SBL)
iko mstari wa mbele kuwekeza katika miradi ya maji safi na salama kwa
mamilioni ya wakazi wa vijijini nchini Tanzania. Miradi hii ya maji
imepewa jina, Water of Life, wenye lengo la kuchochea jumuiya yenye
maendeleo endelevu. Mpango huu umeanishwa kwenye mkakati wake wa
maendeleo wa muda mrefu unaoitwa Society 2030; Spirit of Progress.
Tangu
mwaka 2010, SBL imetumia zaidi ya TZS-1.1bn/- kuchimba visima 18 nchini
kote, jambo ambalo limechangia kupunguza uhaba wa maji nchini. SBL pia
imeshirikiana na mashirika mengine kwenye ujenzi wa miradi hiyo ili
kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata maji safi na salama katika baadhi
ya maeneo yenye uhitaji zaidi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa
Uhusiano wa Kampuni ya SBL, John Wanyancha alisema kuwa SBL inachukulia
maji kuwa jambo muhimu sana kwenye ustawi wa jamii, na ndiyo maana
inashirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo kuwezesha
upatikanaji wa maji safi na salama nchini.
Mwaka huu SBL
ilizindua mradi wa maji wenye thamani ya Tsh milioni 220 katika kijiji
cha Machochwe wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwenye jitihada zake za
kupeleka maji safi na salama vijijini. Mradi huu na uwezo wa kuhudumia
watu zaidi ya 12,000. Mradi huu pia unajumuisha kisima na mifumo yake,
pampu ya maji inayotumia nguvu ya jua na tanki la maji linaloweza kutoa
lita 7,500 za maji kwa saa.
Vilevile SBL imewekeza kwenye mikoa
mingine ya Iringa, Kilimanjaro, Mwanza, Tanga, Ruvuma, Dar es Salaam,
Pwani na Dodoma ikiwapatia wanufaika zaidi ya milioni moja maji safi na
salama. "SBL imeweka sera ya makusudi kusaidia ustawi wa jamii yetu Maji
ikiwa ni mojawapo la maeneo manne ya kipaumbele ambayo kampuni yetu
imeainisha katika malengo yake ya kutoa msaada wa kijamii", alisema
Wanyancha. Alifafanua pia vipaumbele vingine vya kampuni kama utoaji wa
stadi za maisha, utunzaji wa mazingira na elimu juu ya athari ya unywaji
pombe kupita kiasi.
Zaidi ya hayo, miradhi hii ya maji pia
imelenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa nafaka zao kama
vile mahindi, mtama na shayiri ambazo ni malighafi muhimu sana katika
utengenezaji wa bia. Mfano, mwaka 2020 pekee, SBL ilipata tani 17,000 za
nafaka hizi ndani ya nchi, sawa na asilimia 70 ya mahitaji ya mwaka ya
malighafi ya SBL kutoka kwa mtandao wa wakulima 400. Kufikia 2025, SBL
imelenga kuongeza upatikanaji wa malighafi hadi asilimia 85. SBL pia
inasaidia wakulima kwa kuwapa mbegu bure, kuwapa huduma za kiufundi za
shambani na kuwaunganisha na taasisi za kifedha.
Ni jambo
lisilopingika kwamba SBL imeweka hatua madhubuti za kusaidia maendeleo
ya jamii kama kwenye uwekezaji wa maji safi na salama hususani nyakati
hizi za uhitaji mkubwa wa maji nchini. Na kwa wakazi wa vijijini
uwekezaji huu umeleta faraja ukizingatia ya kuwa bado kuna baadhi ya
maeneo upatikanaji wa maji umekuwa mgumu sana na vyanzo vyake kutokuwa
salama kwa afya zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...