Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya MWANGA Bi, Mwajuma Nasombe amezitaka kampuni za ENGEINEERING PLUS na JV PETRA CONTRUCTRACTION LTD zinazojenga Miundombinu ya Umwagiliaji katika Skimu ya Kirya iliyopo Wilayani Mwanga Mkoani Kilimanjaro kuwasilisha mpango mkakati wa ujenzi wa Miundombinu hiyo Ofisini kwakwe, kwa hatua za ufuatiliaji pamoja na kuongeza nguvu kazi, mashine na mitambo inayohitajika ili kuharakisha ujenzi wa Miundombinu hiyo.
Kwa upande wake Mhandisi Juma Hamsini wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji amemshauri mkandarasi kuwashirikisha Wataalam wa Halmashauri, wanakijiji wa Kirya na viongozi wa maeneo mradi unapotekelezwa kwa kuwa wanaijua Geografia ya eneo husika na mazingira yanayowazunguka, suala litakalomsaidia mkandarasi katika kutekeleza wajibu wake wakati huu wa ujenzi.
Mnufaika wa Mradi huo ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya ujenzi Bw, Nyange Laizer ameishukuru serikali kwa mradi huo utakaoboresha maisha ya wafugaji katika kijiji cha Kirya kwa kuongeza pato la familia kupitia kilimo cha Umwagiliaji.
Mhandisi Msimamizi wa Mradi huo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Romwald Robert, amekiri mkandarasi kuwa nyuma ya muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba ambapo ameahidi kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo na kumshauri ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa kasi na kufidia muda ulipotea hatimaye mradi huo ukamilike katika muda uliopangwa.
Ujenzi wa Mfereji Mkuu utawezesha Banio la pili kuanza kufanya kazi na kuongeza eneo la Umwagiliaji kutoka Hekta Mia nne Hamsini (Hekta 450) hadi Hekta Miatisa (Hekta 900) ambapo ujenzi huo unajumuisha barabara yenye urefu wa kilometa 16, vivuko viwili vya Miguu pamoja na Makalavati na unatarajiwa kumalizika katika kipindi cha miezi 8 kwa gharama ya zaidi ya Shillingi Bilioni Moja.
Skimu ya Umwagiliaji ya Kirya ina zaidi ya wanufaika Elfu mbili (2000) wanaolima zao la mpunga na Mbogamboga.
Wahandisi na Wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakitazama Banio la pili litakaloanza kutumika mara baada ya Mfereji Mkuu kukamilika.
Mashine aina ya EXCAVATOR ikichimba Mfereji Mkuu unaotoa Maji kwenye Banio hadi katika Skimu ya Kirya.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga Bi, Mwajuma Nasombe (aliyevaa Miwani) akitoa maelekezo kwa Bw, Nyange Laizer mjumbe wa kamati ya Ujenzi kuhusu wajibu wa jamii ya Kirya kutoa ushirikiano unaohitajika kwa Mkandarasi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...