Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema ujenzi wa bandari ya Kalema wilayani Tanganyika, Mkoa wa Katavi inayogharimu shilingi bilioni 47.9 utafungua fursa ya kukua kwa uchumi wa Mikoa inayopakana na ziwa Tanganyika ukiwemo mkoa wa Katavi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka alipotembelea ujenzi wa bandari hiyo utaokamilika mwezi Machi, 2022 na kwa sasa ujenzi upo asilimia 66.
Akiwa katika mradi huo Shaka amesema CCM itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati kiuchumi itakayoiwezesha Nchi yetu kunufaika na nafasi yake kijiografia ikiwemo kuimarisha huduma za bandari katika ziwa Tanganyika na ujenzi wa bandari ya Kalema ni kielelezo.
Pia, amesisitiza wizara ya ujenzi kutekeleza ujenzi barabara inayokwenda kwenye eneo hili la bandari kwa kiwango cha lami ili kuendana na kasi ya ukamilishaji wa mradi wa bandari hivyo kurahisisha utoaji wa huduma katika eneo hilo.
"Mradi huu ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu na mkoa huu wa Katavi kwani utahuisha na kukuza biashara kati ya nchi yetu na Nchi jirani za DRC, Burundi na Zambia. Niwakumbushe wananchi wa wilaya hii ya Tanganyika kujipanga kunufaika na fursa hizi hivyo wajiepushe na uuzaji hovyo wa ardhi bali wawe wa kwanza kuanza kuchangamkia fursa.
Tutaisukuma wizara ya ujenzi kuipa kipaumbele barabara itakayohudumia bandari hii kujengwa kwa kiwango cha lami katika muda mfupi ili kuendana na kasi ya ujenzi wa bandari hii ili pindi inapokamilika ianze kutoa huduma kikamilifu." Alisema Shaka.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...