Adeladius Makwega,Dodoma.
Nilikuwa nimekaa katika ukumbini Jijini Mbeya huku baadhi ya wapambaji wakiupamba ukumbi huo tayari kwa kilele cha Tuzo za Filamu zilizokuwa zinafanyika jioni ya siku hiyo. Hali ilikuwa ni bize bize kila mmoja na kazi yake ilimradi shughuli hiyo inafana. Katika watu niliyokuwa ninawafahamu ukumbini wakati huo alikuwa ni Joseph Kigingi pekee na alikuwa akipiga piga picha za maandalizi kwa ajili ya shughuli za kihabara za tukio hilo.
Nilikuwa nimekaa katika kiti jirani na sehemu alipo Disco Joker, kwani eneo hilo ndipo nilipoweza kuunganisha kompyuta yangu mpakato na kupata umeme. Disco Joker huyu alikuwa akijaribu vyombo vyake akiwa jirani na binti mmoja mrembo anayefahamika kama Regina, kwa hakika alikuwa mrembo mno, kwa umri wangu mrembo kama huyo nilimuona miaka 16 iliyopita, hapa katikati macho yangu hayajajaliwa kumuona mrembo kama huyo.
Mwanakwetu, unaweza ukaomba Vatikani waitishe mtaguso mwingine alafu waruhusu mitala, ili kupata nafasi ya kuwa na wake wawili. Huku na wewe ukifunga novena ya kimyakimya kuomba ajenda kama hiyo kuwemo katika mtaguso huo.
Nilifanya kazi zangu kwa saa kadhaa, mara nilihisi njaa nikaamua kutoka zangu nje ili niweze kupata chakula cha mchana.
Nilipotoka nje ya ukumbi tu, kwa kando kuna Chuo Kikuu cha Mtakatifu James niliambiwa kuwa eneo hilo linaitwa Mafyati. Nilitoka hadi barabara kuu kama naelekea Mbeya Mjini usawa pembeni ya Chuo Kikuu hiki, nikavuka barabara nikaona kama kuna mtaa unaingia kwa ndani hivi. Kweli nilikuta vijana wakiuza chipsi, ndizi na nyama za kuchoma.
Niliuliza bei nikaambia kuwa ndizi tano 1000/-na nyama 1000/-, nikaupa jina Mwana wa Kabwela Mkahawa niliagiza chakula na kwa kuwa kulikuwa na manyunyu ya mvua siku hiyo, ilikuwa hakuna budi kuingia ndani niketi ili kuandaliwa nilichoagiza.
Nilipoingia ndani ya sehemu
hii ya kuuza chakula nilianza kujifuta matone ya manyunyu ya mvua yaliyonilowesha.
Kabla sijamaliza kujifuta, mara nilisikia…
Natamani
ni nawe kila saa, Usiku na mchana hakuna njaa, Mimi upo pembeni,
Kweli
najivunia,Tabibu ndani yangu, Washa taa, Ndani giza nene, Washa Mshumaa
Sikia
hizi hisia, Karibu ndani, Naumia. Yeeyaa..
Nasame
jambo jambo mama, Habari gani nzuri sana
Ukiniacha
, Nitaumia, Mwenzio nishakuzimia
Without
you without you Nothing I can Be (Mara 2)
Without
you without you No Steve R&B yeeyaa…(Mara 2)
Pale tu nilipousikia wimbo
huo, njaa yangu ilikata na nikaanza kuucheza kwa dakika kama mbili hivi. Vijana
hapa mkahawani wakishangaa mbona mteja wao amefurahishwa sana na wimbo huo?
Wimbo huo uliisha na ukaanza kuchezwa mwingine, nilibaini wimbo wa Jambo Jambo
na hizo zingine zilichezwa na redio moja ya FM hapo Mbeya Mjini.
Akilini mwangu wimbo huo ulinikumbusha mbali sana kati ya mwaka 2013 na 2016 wakati huo TBC Taifa walianzisha kipindi kinaitiwa Habari na Muziki ambacho kilikuwa hewani baada ya Jioni Njema na kikitayarishwa na Angel Mdungu (Sasa yupo DW Kiswahili), Batlet Milanzi (Sasa yupo NKH), Hamisi Holela(Bado yupo TBC Taifa/TBC FM), Farida Hamisi (Yupo TBC International), Frank Kashonde(Yupo Radio Maria), Essero Mafuru(yupo TBC Taifa /TBC 1) na mimi Mwana Wakabwela tukisimamiwa na Mkurugenzi wetu wa Huduma za Redio wa wakati huo Bi Susan Mungi.(Sasa ni Mchungaji)
Nakumbuka kila siku saa 12-1 jioni jumatatu hadi ijumaa tulihakikisha katika orodha za nyimbo zetu (line up ) ya siku angalau wimbo hata mmoja kati ya nyimbo sita za siku zilizokuwa zinachezwa moja lazima ilikuwa ya Stephen Wiliam Gambo (Steve R&B) vibao kama vile Jambo jambo (Steve R&B), One Love (Steve R&B na Baby Boy),Tulikotoka (Steve R&B),Sintomuacha (Steve R&B na Mangawair), Usinihukumu (Steve R&B na Maunda Zorro) na Huyu Demu (Steve R&B Mr Blue).
Nilijiuliza swali, hivi Stephen William Gambo (Steve R&B) yupo wapi? Nilimtafuta Bakar Katumbatu ambaye zamani alikuwa mtayarishaji wa vipindi vya vijana TBC 1, nilimuuliza juu ya Steve R& B yu wapi? Alinijibu kuwa mara ya mwisho aliwasiliana naye akiwa Uturuki.
Kumbuka nipo mkahawani na vijana ndiyo wanaendelea kuandaa chakula. Nilipatiwa namba, nikampigia mwanamuziki huyu, aliniambiwa kuwa sasa hivi muziki unasumbua kwa sababu ya janga la Korona, hawafanya tena maonesho ndani na nje ya nchi, utaratibu wa maisha ya watu umeharibika kabisa.
“Wakati nilipofanya wimbo huu wa Jambo Jambo watu wengi walidhani mimi ni Mkenya, nilipomaliza wimbo huo ndipo nilipata kazi za nje ya nchi, kwa hiyo ni kweli wimbo wangu ulipendwa sana lakini sikuwepo nyumbani na wala sikunufaika kifedha lakini unisaidia kujulikana mno.” Alinidokeza Steve R&B ambaye sasa anafanya kazi na In African Band.
Msanii huyu ambaye ni mzigua wa kutoka Kijiji cha Kabaya Handeni Tanga anadai kuwa alitunga wimbo huu kutokana na rafiki yake mmoja ambayo alikuwa anapenda sana muziki wa Rege alikuwa anamsikilizisha midundo yake na kama ulivyo muziki wa R&B na Rege ina mahusiano ya karibu sana akashawishika kutunga wimbo huo.
“Nilifanya kama utani tu, ulipokamilika ukawavutia sana mashabiki wangu wa Afrika Mashariki na Kati na Ughaibuni.”
Steve R&B ambaye ni
muhitimu
wa Diploma ya IT kutoka chuo cha IFM Dar es Salaam anasema kuwa siku
ya kwanza Jambo Jambo ilichezwa Coco Beach, alimpatia DJ na uliwavutia mno
wapenzi wa muziki.
“Nilishangaa watu walinyanyuka na kucheza kana kwamba ni wimbo maarufu, kumbe nilikuwa nimetoka kuuchukua kwa mtayarishaji (producer), hata nyumbani sikufika, kituo cha kwanza kilikuwa Coco Beach.”Alisema huku akikumbuka mengi ya wakati huo.
Mara nilishikwa begani na
vijana wa mkahawa huo na kunijulisha kuwa chakula changu kipo tayari na nilishangaa
wakati huo huo simu yangu ilikata gafla kwa kuwa ilikuwa imeloana na manyunyu
ya mvua. Nilikula chakula haraka na nilipitia kwa fundi angalau kuitengenza
simu yangu ilipotengemaa nikarudi ukumbini kusubiri kuanza kwa kilele cha Tuzo
za Filamu Disemba 18, 2021.
0717649257
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...