Mwanahabari nguli kupitia kituo cha Azam tv Ramadhan Mvungi akifanya mahojiano ya kina na Mkuu wa Majeshi Tanzania Jenerali Mstaafu Mirisho Sarakikya nyumbani kwake.
Mkuu wa kwanza wa Majeshi Tanzania,Jenerali Mstaafu Mirisho Sarakikya akizungumzia miaka 60 ya Uhuru kwa vyombo vya habari nyumbani kwake Kijiji cha Nkoaranga Wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Mkuu wa kwanza wa Majeshi Tanzania Jenerali Mstaafu Mirisho Sarakikya akiwa na mke wake nyumbani kwake Kijiji cha Nkoaranga Wilayani Arumeru.




Na Pamela Mollel, Arusha

Isingekuwa ni Mlima Kilimanjaro, ulioko Tanzania, Raia wa nchi ya Ethiopia wasingepata Pasipoti za Kusafiria.

Akirejea kumbukumbu zake za miaka 60 ya Uhuru, Mkuu wa kwanza wa Majeshi, Jenerali Mstaafu Mirisho Sarakikya amebainisha kuwa, Mlima Kilimanjaro ndio ulikuwa chachu ya kuifanya serikali ya Ethiopia kuanza kutoa hati za kusafiria kwa ajili ya wananchi wake kuja Tanzania kufanya utalii kuupanda mlima huo.

“Pasi za kwanza za kusafiria kwa raia wa Ethiopia zilitolewa maalum kwa ajili ya watu kutoka nchi hiyo kuja kufanya utalii wa kupanda Mlima Kilimanjaro,” alisema Jenerali huyo Mstaafu.

Akizungumza nyumbani kwake kijijini Nkoaranga, Wilayani Arumeru, Mkoani Arusha, aliyekuwa Mkuu wa kwanza wa Majeshi, Jenerali Mstaafu Mirisho Sarakikya amefafanua kuwa yeye ndiye aliyeishawishi serikali ya Ethiopia kuanza kutoa pasipoti kwa raia wa kawaida ili waweze kuja Tanzania kupanda Mlima Kilimanjaro, kipindi akiwa balozi nchini humo miaka ya mwanzo ya 80.

Awali, serikali ya Ethiopia iligoma kutoa pasi za kusafiria kwa wananchi wake, ikihofia kwamba wangetoroka nchini humo kwenda kutafuta maisha sehemu zingine duniani.

“Nilijenga urafiki na mkuu wa idara ya uhamiaji nchini Ethiopia na kuanza kumshawishi awaruhusu watu wake waje Tanzania kupanda mlima mrefu kuliko yote barani Afrika,” alisema Jenerali Sarakikya.

Hata hivyo makubaliano ya awali yalikuwa kwamba, raia wa Ethiopia wakitua katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, basi pasi hizo zichukuliwe na kuhifadhiwa hadi wakati wa wao kurudi ndipo wakabidhiwe tena.

“Na hata hivyo tuliwaonya kwamba wasijaribu kuzitumia pasi hizo vibaya kwani wangewaharibia na wenzao walioko Ethiopia.” Alisema Sarakikya.

Baada ya hapo, Raia wengi wa Ethiopia walifanikiwa kupata pasi za kusafiria na wengi wamesambaa duniani kote na huwa wanakumbuka jinsi Mlima Kilimanjaro ulivyowasaidia kuwapa fursa ya kutoka nchini mwao.

“Wengi huwa wananipigia simu hadi leo wakishukuru kwa kuwafungulia njia kupitia mlima Kilimanjaro!” Alimalizia.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...